Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAHAMASISHA MATUMIZI YA VIFUNGASHIO VYA MKONGE

Wajumbe wateule wanaounda kamati ndogo ya Mkonge

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo ndogo kwaajili ya kuboresha zao la Mkonge

**************************

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

SERIKALI imeanza kutumia na kuhamasisha matumizi ya vifungashio vitokanavyo na zao la Mkonge kwenye bidhaa za mazao ya kimkakati.

Hatua hiyo imekuja baada ya kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), katika kamba zinazozalishwa kwa kutumia mkonge (katani).

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema hayo leo Julai 16,2022 wakati wa uzinduzi wa Kamati Ndogo ya Mkonge yenye wajumbe 11 ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima.

Chini ya uenyekiti wa Malima, akisaidiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella wakishirikiana na wataalamu mbalimbali kutoka wizara hiyo kamati hiyo itaisaidia serikali kufikia malengo.

Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni Magid Mwanga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Edward Mpogolo Mkuu wa Wilaya ya Same, Gullam Dewji, Mwenyekiti MeTL, Saddy Kambona Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Mkonge Tanzania, Dk. Catherine Faustin Senkoro, Mkurugenzi TARI Mlingano na Naweed Mulla, Mkurugenzi Mtendaji Highland Estate.

Wengine ni Enock Nyasebwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Elizabeth Kalambo, Mtendaji Mkuu Sisalana (T) Co. Ltd na Shadrack Lugendo, Mwenyekiti Magunga Amcos.

Waziri Bashe amesema ofisi yake imeamua kufanya maamuzi kwamba hawatatumia vifungashio vingine zaidi ya katani katika bidhaa mbalimbali ili kulinda soko la mkonge na kutunza mazingira hapa nchini.

Asema wameamua kuanza na mazao ya kimkakati ambayo yatatumia vifungashio vya katani na kuyataja kuwa ni Korosho, Pamba, Kahawa na mengineyo.

“Baada ya kufanya maamuzi ya kisera sisi kama wizara na mwaka huu tumefanya mabadiliko kwenye kodi, tumefuta kodi ya VAT katika kamba zinazozalishwa kwa kutumia katani na kwenye magunia yanayozalishwa ndani ya nchi.

“Kwa sababu kama nchi kwenye zao la korosho pekee yake tunaagiza kutoka nje gunia zenye thamani ya Sh bilioni 18 kwa mwaka, halafu unavyoagiza unampa yule mzalishaji msamaha wa kodi ya kuingiza bidhaa. Kwa hiyo tuliamua kwamba tunaanza kufanya maamuzi kama wizara kuchagua mazao ambayo hatutatumia vifungashio vingine isipokuwa vya katani.

“Mojawapo tumeanza na korosho mwaka huu na kiwanda cha magunia hapa Morogoro kimeanza kazi tutoa oda ya gunia milioni nne ingawa uwezo wake ni kutengeneza magunia milioni 10 ambayo mwakani tutampa yote hayo anayoweza kuzalisha ili gunia ziweze kufanya kazi,” amesema Bashe.

Post a Comment

0 Comments