Ticker

6/recent/ticker-posts

TARURA YALETA FARAJA KWA WANANCHI MOMBA


**********

Wananchi Wilayani Momba, Songwe wanefarijika baada ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa daraja la muda katika mto Nkana Kata ya Chilulumo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya daraja la awali kuvunjika na kusababisha mawasiliano ya Kata za Chilulumo,Nkulwe,Kamsamba,Mkomba Ivuna na makao makuu ya Wilaya ya Momba kukatika.

Akitoa taarifa kwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TARURA, wakati wa ziara yao mkoani Songwe, Meneja wa TARURA Mkoa wa Songwe Mhandisi Killian Haule alisema kuwa TARURA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Songwe,Jeshii la wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamejipanga kurejesha mawasiliano ndani ya muda mfupi kwa kujenga daraja la chuma (TRUSS Bridge) ili wananchi wapate huduma ya Usafiri na Usafirishaji.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA Mhandisi Florian Kabaka amesema kuwa daraja hilo ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi na amewataka wananchi kulitunza pindi litakapo kamilika.

Mkurugenzi wa barabara kutoka TARURA Mhandisi Venant Komba ameeleza kuwa licha ya ujenzi wa daraja la muda, TARURA inafanya maandalizi ya ujenzi wa Daraja la kudumu katika mto Nkana.

"Maandalizi ya ujenzi wa daraja la kudumu hapa mto Nkana yanaendelea maana eneo hili ni muhimu sana kwa wananchii ili kuwawezesha kusafirisha mazao hasa zao la mpunga,” alisema mhandisi Komba.

Kwa upande wake Mhe. Sabasi Semfukwe, diwani wa kata ya Chitete alisema kuwa walikuwa wanapata changamoto kubwa sana kutokana daraja kuvunjia, kwa kuzingatia kuwa njia hiyo ni ya kimkakati kwa ukuaji wa uchumi wa maeneo yao.

“ Tumefarijika sana sababu kujengwa kwa daraja hili kwetu ni kufungua ukuaji wa kiuchumi kwa kusafisha mazao yetu. Mawasiliano sasa yatakuwepo na itaongeza tija kwa wananchi katika maswala ya uzalishaji,” alisema Mhe. Semfukwe.

Naye Rehema Kipubile mkazi wa Kanyala alisema kuwa anaishukuru Serikali kwa kuwaletea daraja hilo kwani wamepata tabu sana baada ya mawasiliano kukatika kuzifikia huduma muhimu za kijamii.

“Sisi wakinamama hasa tukiwa wajawazito tumepata tabu sana kuvuka hapa kwenda hospitali, tunashukuru sana kwa daraja hili jipya linalojengwa tutapata nafuu, “ alisema Rehema

Bodi ya Ushauri ya TARURA imekamilisha ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi katika Mikoa ya Iringa,Mbeya na Songwe ambapo imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi na kuleta matokeo chanya ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa wakala

Post a Comment

0 Comments