Ticker

6/recent/ticker-posts

UGANDA YAFIKIRIA KUTUMIA BANDARI YA TANGA KUPITIA KAMPUNI YA GBP.*****************************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.


NCHI ya Uganda inaangalia namna ya kutumia bandari ya Tanga kupitia kampuni ya GBP kuagiza mafuta yao yatakayoweza kusafirishwa kwa njia ya barabara au reli.
Waziri wa nchi anayeshuhulikia maendeleo ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini Uganda, Peter Lokeris ameyasema hayo wakati wakiwa katika Kampuni ya mafuta ya GBP jijini Tanga walipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta kutokea Ohima nchini Uganda kija Chongoleani jijini Tanga .


Waziri Lokeris amesema wao kama nchi waamini hatua hiyo itasaidia kurahisisha kwenye uingizaji wa mafuta tofauti na njia wanayoitumia kwa sasa, kwasababu wao pia wanazalisha bidhaa nyingi hivyo itawawezesha na wao kusafirisha bidhaa zingine kutoka nchini Uganda na kuja Tanzania na kwamba hatua hiyo itaimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili huku akiitaka kampuni ya GBP kuwekeza nchini Uganda.


"Kwanza kabisa niipongeze kampuni ya GBP kwa namna walivyowekeza Nchini Tanzania huu ni mfano wa makampuni mengine kuiga sisi Unganda tunakaribisha sana GBP kuja kuwekeza tukiahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha kwenye uwekezaji wao, " amesema Waziri huyo.


Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya GBP Badar Sood amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha sekta binafsi kuwekeza bila vikwazo vyovyote, jambo ambalo limekuwa likileta maendeleo ya nchi hali inayopelekea kuongezeka kwa wageni wengi kutoka nje ya nchi.


"Tumepokea ugeni huu kutoka nchini Uganda pamoja na viongozi wetu wa wizara ya nchini wakiongozwa na katibu mkuu Wizara ya Nishati na Madini Felchesmi Mramba, kimsingi tunashukuru kwa pongezi ambazo wametupatia kwajili ya uwekezaji hapa hivyo tunawakaribisha kuwekeza kufanya biashara kwa pamoja kwakweli wameridhishwa na wapo tayari kutumia GBP Tanga Terminal kwajili ya upokeaji wa mafuta ya kwenda Uganda ambayo yatasafirishwa kwa njia ya meli, reli au barabara " amebainisha Badar.


Aidha ameishukuru serikali ya Uganda kwa kuwakaribisha kwenda kuwekeza nchini humo na kueleza kuwa wanategema kufanya biashara kwa maslahi ya pande zote mbili.


Naye Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya nishati Dastan Kitandula amesema kuwa ujio huo una mafanikio na manufaa makubwa kama inavyofahamika nchi hizo mbili zimeingia kwenye makubaliano ya kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka nchini Uganda kuja Chongoleani Tanga ili kuwawezesha wadau kuuza mafuta yao nje ya bara lao.


"Kazi kubwa inayofanyika hivi sasa ni ya uwekezaji mkubwa ambao unatarajiwa kuleta manufaa kwa Tanzania na wenzetu wa Uganda lakini kama mnavyofahamu mafuta haya bado hayajasafishwa lakini wenzetu vilevile wanahitaji mafuta ambayo yamesafishwa kwahiyo wameona fursa ya kuendelea kuitumia bandari yetu ya Tanga kupokea mafuta ambayo hayajasafishwa kutoka nje yapitie Tanga ili yaweze kupelekwa Uganda, " amesema Kitandula.


"Kama mlivyosikia wenyewe wamewakaribisha GBP waweze kwende kuwekeza Nchini Uganda na tayari GBP wanafanya biashara na Uganda ya kusafirisha mafuta yao nadhani hii ni fursa sasa nzuri sana ya kuendelea kuimarisha uwekezaji kati ya pande zote mbili hivyo nichukue fursa hii kuipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika Nchi yetu mazingira ambayo yanavutia sekta binafsi kuweza kuwekeza na kufanya biashara hali inayoongeza uchumi wa nchi, faida kwa watanzania kupata ajira na wenzetu wa Uganda nao kuweza kupata mafuta ambayo ni ya bei ya chini, " amesisitiza Kitandula.


Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amemshuru Rais kwa kubwa anayoendelea kuifanya na kueleza kuwa serikali ya Rais Samia imeendelea kuweka nguvu kubwa katika mradi wa bomba la mafuta na kwamba wamejionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na kampuni ya GBP na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uchumi wa Tanga na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments