
*************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda leo Julai 28,2022 amefanya ziara ya kutembelea Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kujionea ukuzaji wa teknolojia kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo mara nyingi hutengenezwa nje ya nchi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha kujifunzia DIT, Waziri Mkenda amesema kuwa teknolojia ambazo wamekuwa wakiibuni DIT wanatakiwa waangalie uwezekano kuibiasharisha na baadae kuiingiza sokoni.
Amesema amejionea ni namna gani DIT wanatengeneza vipuri ambavyo vinatumiwa hasa kwenye bajaji na pikipiki na hata kwa baadhi ya magari na kufungua milango ya kufanya uhamisho wa teknolojia kutoka nje kwa kujifunza hapa nchini na kuibiasharisha.
Vipuri hivyo wanatengeneza kwa kutumia chupa za plastiki ambazo zimetupwa na kuzichukua kuziyeyusha na kutengeneza piletes ambazo zinasaidia kutengeneza vipuri hivyo ambavyo hutumika kwenye pikipiki,bajaji na hata kwenye magari.
Amepongeza uongozi wa Chuo hicho kuendelea kuibua bunifu mbalimbali ambazo zitakuwa msaada mkubwa kwa vijana na taifa kwa ujumla kwani kunaweza kusaidia kuokoa fedha nyingi za kigeni.
"Tukiendelea hivi, baadae tunaweza kusema tuzalishe pikipiki zetu, tusikimbilie kusema tunazalisha pikipiki, wenzetu India na China walianza hivihivi kabla ya kuanza kutengeneza pikipiki na magari. Leo mnatengeneza vipuri baadae tutaweza kutengeneza pikipiki zetu". Amesema Waziri Mkenda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, (DIT) Mhandisi Dkt.Richard Masika amesema Taasisi ya Teknolojia kwa muda mrefu imekuwa ikitoa elimu nadharia zaidi baada ya hapo ikaweka msisitizo mkubwa kwa vitendo lakini wameona kwamba pamoja na kufanya hivyo bado wahitimu wamekuwa wanaajirika lakini hawawezi kujiajiri, kwahiyo wameona waende kwenye hatua nyingi kwa kuwafunza wanafunzi kwa kuwatengenezea mazingira ya kiwanda na kufanya kazi za uzalishaji kwenye kiwanda hatua kwa hatua na zile bidhaa zinazotoka zinakwenda kutumika.
Pamoja na hayo amesema kiwanda hicho kinazalisha bidhaa za aina saba tofauti, uzaloishaji wake unategemeana zaidi na oda wanazokuwa nazo, bidhaa zinazozalishwa huchukuliwa hapo hapo na kwasasa watumiaji wengi wameshawafahamu na wanakwenda moja kwa moja hapo chuoni kuchukua bidhaa hizo
Amesema wanachokifanya sasa ni kuyaweka vizuri mazingira ya uzalishaji ili kiwanda hicho kiwe halisi cha uzalishaji hivyo kumsaidia mwanafunzi anapotoka hapo anakuwa tayari kuingia kiwandani bila hofu yoyote
"Kwa mwaka huu tumepanga kuzindua viwanda viwili, kiwanda kimoja ni hiki ambacho tunakifanyia majaribio na kiwanda cha pili kitakuwa Mwanza ambacho kitakuwa kinazalisha bidhaa za ngozi na itaanzia kwenye hatua ya chini kwa maana ya kuitibu ile ngozi na kuikausha na baadae kutengeneza bidhaa nyingi zaidi". Amesema Mhandisi Dkt.Masika.













(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
0 Comments