Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MULAMULA ASHIRIKI MKUTANO WA 41 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA UMOJA WA AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaoendelea jijini Lusaka, Zambia. Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) ukiendelea jijini Lusaka, Zambia Picha ya pamoja ya Mawaziri, Viongozi waandamizi wa Serikali, Taasisi mbalimbali za Kimataifa na Watendaji wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea jijini Lusaka, Zambia.

************************

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) yupo jijini Lusaka, Zambia kushiriki Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza leo tarehe 14 jijini humo.

Mkutano huo wa siku mbili umepokea na kujadili taarifa za kiutendaji za Taasisi za Umoja wa Afrika ikiwemo Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (Mabalozi) kwenye Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Afrika katika kipindi cha Februari-Juni 2022.

Mkutano huo pia utapitisha Bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2023 pamoja na bajeti ya kifungu cha utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika yaliyopitisha Kiswahili kuwa Lugha ya Kazi ya Umoja huo.

Katika mkutano huo Waziri Mulamula anatazamia kusisitiza Kamisheni ya Umoja wa Afrika kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa maamuzi ya Kiswahili kuwa Lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika, kuhimiza matumizi sahihi ya rasilimali fedha na kusisitiza umuhimu wa uwazi na usawa kwenye mchakato wa ajira ili kuwezesha Watanzania kupata ajira kwenye umoja huo.

Mkutano huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje utafuatiwa na Mkutano wa 4 wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 17 Julai 2022.

Kamati hiyo inaundwa na nchi za Senegal (Mwenyekiti); Libya (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti); Angola (Makamu wa Tatu wa Mwenyekiti); Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Katibu) na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya za Kikanda za Umoja wa Afrika.

Umoja wa Afrika una Jumuiya nane za kikanda ambazo ni Arab Maghreb Union (AMA), COMESA, Community of Sahel-Saharan States (CEN-SAD), EAC, ECCAS, IGAD na SADC.

Waziri Mulamula katika Mkutano huo ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Hassan Simba Yahya, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Shiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi wa Sheria Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Balozi Caroline Chipeta na Maafisa wengine Waandamizi.

Post a Comment

0 Comments