Ticker

6/recent/ticker-posts

MAANDALIZI JUBILEI MIAKA 50 SINGIDA YASHIKA KASI

Timu ya Mapadri wa Jimbo Katoliki Singida ikiwa kwenye picha ya pamoja muda mfupi kabla ya mchezo wao wa soka dhidi ya Walei jimboni humo. Mchezo huo ulilenga kutoa hamasa na kuchagiza upendo, furaha na amani kama maandalizi kuelekea kilele cha sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki Singida ifikapo Agosti 21 mwaka huu.
Timu ya Walei Jimbo Katoliki la Singida kabla ya mechi yao dhidi ya mapadri jimboni humo hivi karibuni.
Timu ya Masista wakivuta kamba dhidi ya Wakinamama Wakatoliki Tanazania jimboni humo (WAWATA) katika tamasha la michezo kuelekea kilele cha Jubilei.
WAWATA wakionyesha umwamba wao dhidi ya masista kwenye mchezo wa kuvuta kamba uliofanyika hivi karibuni ndani ya uwanja vya LITI Stadium Mkoani hapa.
. Mapadri wakichuana vikali dhidi ya Walei kwenye mchezo wa kuvuta kamba.
Walei wakijitahidi kuibuka na ushindi dhidi ya mapadri kwenye mchezo wa kuvuta kamba.
Mhasibu wa Jimbo Katoliki Singida Padri Bernard Ngalya akionyesha umahiri kwa kudaka penati iliyopigwa na Makamu wa Askofu wa Jimbo hilo Padri Francis Limu wakati akizindua tamasha hilo.
Watazamaji wakifuatilia tamasha hilo la hamasa kuelekea kilele cha jubilei ya miaka 50 Jimboni Katoliki Singida.
Sherehe zikiendelea.
Sherehe zikiendelea.
Makamu wa Askofu Pd. Francis Limu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya waumini kwenye tamasha hilo.
Makamu wa Askofu Pd. Francis Limu akisimamia sheria, kanuni na taratibu ipasavyo kwenye mwenendo mzima wa tamasha hilo.


********************

Na Godwin Myovela, Singida

MAANDALIZI yaliyosheheni shamrashamra za hamasa kuelekea kilele cha Jubilei ya miaka 50 Jimbo Katoliki Singida ifikapo Agosti 21 mwaka huu yamezidi kushika kasi, ambapo moja ya tukio la kuvutia ni namna timu ya mapadri walivyoonesha vipaji vya aina yake kwenye kucheza mpira wa soka kati yao na walei ndani ya uwanja wa Liti mkoani hapa, na hatimaye kufanikiwa kuichapa timu ya walei mabao 5-2.

Kuvuta kamba kati ya timu ya Masista na Wakinamama Wakatoliki Tanzania (WAWATA) ulikuwa ni mchezo mwingine uliotikisa maandalizi hayo na kuleta ushindani mkali huku shangwe zikitawala uwanja mzima-lakini hata hivyo mwishoni kabisa masista walishindwa kutetea ushindi huo kwa 2-1.

Michezo mingine iliyotawala tamasha hilo kuelekea jubilei ilikuwa ni mchezo wa kuvuta kamba kati ya mapadri na walei, kufukuza kuku na ule wa soka uliodumu kwa dakika 90, ambao kabla ya kuanza ulizinduliwa kwa penati nzuri iliyopigwa na Makamu wa Askofu Pd Francis Limu, ambayo hata hivyo penati hiyo ilifanikiwa kudakwa kwa mbwembwe na Mhasibu wa Jimbo hilo Pd Bernard Ngalya.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa tamasha hilo Pd Limu alisema lengo hasa la michezo hiyo sio mashindano bali ni kuhamasisha kuelekea jubilei na kuonyesha umoja na mapendo kati ya wakristu wa Taifa la Mungu ndani ya Jimbo hilo kwa kuzingatia michezo inaleta furaha, amani na inajenga nguvu.

“Nawaalika wote siku ya Agosti 21 ambayo ndio kilele cha Jubilei, na tunatarajia siku hiyo kupata ugeni mkubwa nchi nzima, wakiwemo viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na wote wenye mapenzi mema kuja kushiriki nasi katika kusherehekea jubilei ya miaka 50 ya Jimbo letu la Singida,” alisema Pd Limu.

Hata hivyo, Mhasibu wa Jimbo hilo Pd Ngalya pamoja na kumshukuru Mungu na kuzidi kuomba baraka kufuatia mwenendo mzuri wa maandalizi kupitia kamati husika unavyoendelea mpaka sasa, alisema kwa hakika miaka 50 ni miaka ya kujivunia.

“Kama Jimbo ndani ya miaka hii limefanya mengi katika nyanja mbalimbali, ikiwemo utume kupitia huduma za afya, elimu na mambo mbalimbali ya kijamii…tuna kila sababu ya kushangilia jubilei yetu, leo tumefurahi kwenye Misa Takatifu na tunafurahi pia kwenye michezo hapa uwanjani. Naamini basi, Mungu anazidi kutubariki kuelekea Jubilei yetu ambayo inabebwa na kauli isemayo JUBILEI SINGIDA-UMOJA NA MAPENDO,” alisema Pd. Ngalya.

Post a Comment

0 Comments