Ticker

6/recent/ticker-posts

TASAF YAGUSA MAISHA YA WANANCHI KIJIJI CHA KITANGA KWA KUWAJENGEA VISIMA VYA MAJI SAFI NA SALAMA


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akichota maji kwenye kisima kilichojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya kuwahudumia wananchi mara baada ya kukagua kisima hicho katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe mkoani Pwani.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimtwika ndoo ya maji mwananchi wa Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe mkoani Pwani mara baada ya kukagua kisima hicho kilichojengwa na TASAF katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe mkoani Pwani.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walengwa wa TASAF wa na wananchi wa Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe mara baada ya kukagua kisima kilichojengwa na TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya ya Kisarawe.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ya Kijiji cha Kitanga iliyokuwa ikiwasilishwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Bw. Steven Michael wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Kisarawe.

*****************************

Na. James K. Mwanamyoto-Kisarawe

Tarehe 04 Agosti, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imegusa maisha ya wananchi wa Kijiji cha Kitanga, wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa kujenga visima vya maji safi na salama vinavyotatua changamoto ya ukosefu wa maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza na wanachi wa Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe leo, Mhe. Ndejembi ameipongeza TASAF na wananchi wa Kijiji hicho kwa ushirikiano uliowezesha kukamilika kwa visima hivyo ambavyo hivi sasa vinatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo.

Mhe. Ndejembi amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuhakikisha wanavitunza visima hivyo ili viendelee kuwa msaada kwa wananchi wa eneo hilo kwa kipindi kirefu kama Serikali ilivyokusudia.

“Serikali imewajengea visima hivi, sasa ni jukumu lenu kuvitunza ili navyo vitutunze badala ya kuiachia TASAF na Serikali ya Kijiji jukumu hilo.” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, wanaojua umuhimu wa visima hivyo ni wananchi wa Kijiji cha Kitanga, hivyo Serikali haitofurahishwa kusikia baada ya miaka michache ijayo vimehaibika kwa kukosa matunzo.

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Kitanga, Bi. Fatuma Bozi amesema kabla ya TASAF kuwajengea visima, walikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwani walikuwa wakichota maji yaliyotuama ambayo yalikuwa yakitiririka kutoka bondeni, hivyo wanaishukuru Serikali kwa kuwajengea visima hivyo.

Mhe. Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF mkoani Pwani baada ya kutembelea Wilaya ya Bagamoyo na Kisarawe.

Post a Comment

0 Comments