Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO KUTUA MWANZA KWA ZIARA YA SIKU TATU

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw.Adam Malima akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake.

*******************

Na Sheila Katikula, Mwanza

MAKAMU wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajia kufanya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Mwanza kuanzia Septemba 12 hadi 14 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima ametoa taarifa hiyo leo Septemba 10 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake na kueleza katika ziara yake Makamu wa Rais anatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali mkoani hapa.

Malima amesema Septemba 13 Makamu wa Rais atatembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Sekou Toure na stendi ya kisasa ya Mabasi iliyopo kwenye halmashauri ya Ilemele Kata ya Nyamhongoro.

Malima amesema pia Makamu wa Rais anatarajiwa kuzindua jengo la wodi ya Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

"Tunafahamu huduma zitakazotolewa kwenye jengo hili ni matibabu kwa njia ya mionzi (radio therapy), dawa za kinyuklia na huduma ya kulazwa wagonjwa.

Ameongeza, Dkt. Mpango atazindua jengo la mama na mtoto lenye thamani ya sh bilioni 10.1 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure ambapo mradi huo utaboresha huduma ya afya kwa wananchi hususani mama na watoto na kupunguza vifo wakati wa kujifungua.

Ameeleza, Makamu wa Rais anatarajia kuzindua stendi ya kisasa ya mabasi, maegesho na malori katika Kata ya Nyamuhongoro yenye thamani ya Sh. bilioni 26.6.

"Stendi hii itaongeza mapato ya halmashauri ambapo inakadiliwa kukusanya sh bilioni 2.2 kwa mwaka na itavutia wawekezaji, kuongeza idadi ya wafanyabiashara kwenye halmashauri ya hii na kuboresha mazingira ya usafiri nausafirishaji wa abiria",amesema Malima.

Malima amesema Septemba 14 Makamu wa Rais anatarajia kuweka jiwe la msingi kwenye chanzo cha maji - Butimba kitakachogharimu Sh bilioni 69.3 kwani utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 40.

"Mradi huu unasimamiwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), utazalisha lita milioni 48 kwa siku utaboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi kwa wakazi 450,000 wa mkoani Mwanza.

Post a Comment

0 Comments