Ticker

6/recent/ticker-posts

MICHUANO YA BANDARI KUTIMUA VUMBI SEPTEMBA 26 MOROGORO


********** 

MASHINDANO yanayoshirikisha timu za Bandari maarufu kama Bandari Interports yanatarajiwa kuanza 'kutimua vumbi' kuanzia Septemba 26 mkoani Morogoro na kuwashirikisha zaidi ya wanamichezo 500. 

Akizungumzia mashindano hayo katika kituo cha Televisheni cha TBC Taifa, msemaji wa kamati ya michezo ya Bandari Enock Bwigane amesema michuano hiyo ya kila mwaka pamoja na mambo mengine lengo lake ni kujenga afya za washiriki pamoja na kudumisha ujirani mwema. 

Amesema mashindano hayo yenye zaidi ya miaka 40 tangia kuanzishwa kwake wakati wa uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yatafanyika mkoani humo kwa kipindi cha mwaka wa tatu mfululizo tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa ikiandaliwa katika mikoa tofauti tofauti. 

Amesema awali mashindano hayo wakati wa uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yalikuwa yakizishirikisha timu kutoka Bandari ya Mombasa, Tanga pamoja na Dar es Salaam na baadae kuunda timu moja iliyokuwa ikishiriki michuano mbalimbali. 

Aidha amesema mashindano hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa Oktoba 3 yanawashirikisha timu nane kutoka Zanzibar, TICTS, Shirika la Meli ( MSCL), Makao makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na Bandari za Maziwa zikijumuisha Mwanza, Kigoma na Kyela. " Tunaushukuru uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania chini ya Mkurugenzi Presduce Mkeli Mbossa pamoja Bodi ya Wakurugenzi kwa kuendelea kufanikisha mashindano haya ya kila Mwaka ambapo kufanyika kwake pia kunasaidia kuongeza hari za kazi kwa watumishi" amesema Bwigane 

Kwa Upande wake Mratibu wa Mashindano hayo Kenny Mwaisabula "Mzazi" amesema kimsingi maandalizi ya mashindano hayo yameshakamilika hadi kufikia hivi sasa na kinachosubiriwa ni kwa timu kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kuonyeshana ubabe na bingwa wa mashindano hayo apatikane. 

Amesema michezo inayotarajiwa kutimua vumbi katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na mpira wa miguu, basketball, netball, riadha, Bao pamoja na mchezo wa kuvuta kamba. 

Naye Mjumbe wa kamati ya Mashindano hayo Patrick Kusiga amezitaja faida za mashindano hayo kuwa ni pamoja na uibuaji wa vipaji vya wanamichezo mbalimbali wakiwemo wachezaji Salvatory Edward, Maulid Hussein (machinga) aliyetokea Bandari ya Mtwara pamoja na Bondia Hassan Kinyogori.

Post a Comment

0 Comments