Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA CHINA ZA ADHIMISHA URAFIKI WA ZAIDI YA MIAKA 50 KWA MASHINDANO YA MPIRA WA MEZA


*************************

Na Shamimu Nyaki - WUSM

Tanzania na China zimeadhimisha urafiki wa miaka zaidi ya 50 ambao umeleta mafanikio katika Sekta mbalimbali ikiwemo Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu Saidi Yakubu ameiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya kirafiki ya Mpira wa Meza (Table Tennis) yaliyofanyika Septemba 04, Diamond Jubilee Dar es Salaam ambapo amesema, Tanzania na China zimekua mfano wa Mataifa rafiki Duniani ambayo yamekuza ushirikiano katika maendeleo.

Amesema, mchezo wa mpira wa meza ni miongoni mwa michezo inayokua hapa nchini, na Serikali inaendelea kuwekeza katika mchezo huo ambao unakuza vipaji na kutengeneza ajira kwa vijana.

"Mpira wa Meza unachezwa sana na wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari, na katika Mashindano ya Michezo kwa shule hizo pamoja na Vyuo vya Ualimu na Taasisi za Umma pia unachezwa na unaleta ushindani Mkubwa, hivyo ni miongoni mwa michezo inayotangaza nchi vyema" alisema Ndugu Saidi Yakubu.

Ametumia nafasi hiyo kuliagiza Baraza la Michezo nchini, kukaa na Ubalozi wa China kushirikiana na kuratibu kwa karibu zaidi matukio yote ya michezo yanayoshirikisha nchi hizo, ili kuweza kupata wachezaji wengi zaidi watakaoshindana.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Mhe. Chen Ming Jian ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano katika masuala mbalimbali, huku akiahidi kudumisha urafiki huo katika Sekta ya Utamaduni na Michezo.

Mhe.Chen Ming Jian amesema China imedhamiria kujenga kiwanda Cha kuzalisha filamu, kubadilishana wataalamu katika sekta ya Michezo na Utamaduni na imeahidi kushiriki katika Tamasha la 41 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.

Mashindano hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Umoja wa wacheza mpira wa Meza Tanzania na China pamoja na kituo cha Utamaduni cha China.

Post a Comment

0 Comments