Ticker

6/recent/ticker-posts

WENYEVITI WA VIJIJI WANAOUZA MAENEO ZAIDI YA EKARI 50 KUKIONA CHA MOTO.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akisalimiana na uongozi wa Ccm Wilaya ya Kilindi alipotembelea ofisini hapo kusaini kitabu cha wageni.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Idrisa Mgaza akiongea kwenye kikao cha baraza kabla ya kumkaribisha mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba kulia, kuongea na kujitambulisha kwa madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akiongea jambo na mkuu wa Wilaya ya Kilindi Abel Busalama wakati wa mkutano wa hadhara.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akipewa maelezo na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Gracian Makota.

**************************

Na Hamida Kamchalla, KILINDI.


MKUU wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba amewakalia kooni wenyeviti wa vijiji ambao wanauza maeneo ya wananchi bila ridhaa yao lakini pia ambao hawatoi taarifa ya kipindi cha robo tatu ya mwaka kwa wananchi wao.


Mgumba ameyasema hayo leo alipofanya ziara yake ya kutambuana na viongozi na watumishi wa halmashauri ya Kilindi, alifafanua kuhusu suala la mgogoro wa mipaka uliopo kati ya Wilaya mbili za Kilindi na Handeni, lakini pia mgogoro wa Mkoa wa Tanga na Manyara, kwa Wilaya za Kilindi na Kiteto.


"Nimekuja kuwasalimia sijakuja kikazi ila, mwenyekiti aliyeingia au kuwepo madarakani kwa ajili ya kuuza ardhi ya wananchi bila ridhaa ya wananchi wenyewe, imekula kwake, na wenyeviti wote wasiosoma taarifa kwa wananchi kila baada ya robo, kwa mujibu wa sheria, hawa hawana nafasi kwenye uongozi wa Rais Samia Sulluhu Hassan" amesema."Kwa sababu tunapoelekea fedha nyingi huko kwenye vijiji na zile fedha ni za wananchi na sheria inaelekeza kila baada ya miezi mitatu mwenyekiti wa kijiji atoe taarifa ya fedha kwa wanakijiji wenye fedha zao" amesisitiza.


Pia amefafanua kwamba kwa mwenyekiti au mwananchi ambaye anamiliki mashamba makubwa yanatakiwa yasizidi ekari 50 na endapo yatazidi yatakuwa ni mali ya serikali huku akisema sheria hiyo ndiyo inayotumika kuwabana wenyeviti wa vijiji.


"Kwa mwananchi aliyenunua ardhi, najua huku Kuna wenyeviti wanaouza ardhi maeneo makubwa kinyume cha utaratibu, kijiji kwa mujibu wa sheria namba 5 ya ardhi ya vijiji na namba 4 ya ardhi ya mwaka 1999, kijiji hakina mamlaka ya kugawa ardhi zaidi ya ekari 50" amesema.


"Lakini wenyeviti wa vijiji wa huku wameuza zaidi ya ekari 200, na kuna mtu anamiliki ardhi anadai amemilikishwa na kijiji, kama kuna mtu amemilikishwa na kijiji zaidi ya ekari 50, ataendelea kubaki na hizo tu, zitazobaki zote zitakuwa ni mali ya kijiji husika" ameongeza


Mgumba amesema kuwa wakati mwengine wananchi wanaingia kwenye migogoro isiyokuwa na maana yoyote isiyokuwa na maana na kwamba wanaleta migogoro ni viongozi kwa kutaka maeneo makubwa ili wapate kuyauza na siyo kwa manufaa ya wananchi wao.


"Nawashangaa viongozi wenzangu wanaotoka maeneo makubwa sijui ya nini, na wanaoleta migogoro hii siyo viongozi wakubwa, bali ni wenyeviti wa vijiji vyetu, na wanayataka yale maeneo siyo kwa kuwatumikia wananchi bali kuuza ardhi ya wananchi" amefafanua.


Aidha Mgumba amebainisha kwamba suala la mpaka wa Kilindi na Handeni, Rais ameshalifanyia kazi kwa kutoa maelekezo ya kuundwa kamati ambayo imeshafanyika kazi hivyo inasubiriwa kufika katika meza yake ili atoe maamuzi yatakayotolewa."Baada ya ijumaa Septemba 11 nitawapa taarifa ni siku gani nitakuja na timu yangu na kutatua mgogoro ule, na tutawakutanisha na watu wa Handeni na siku hiyo ndio mgogoro utakuwa umeisha na ndani ya wiki mbili utakuwa ni historia, kila mmoja atakua mpaka unaishia wapi" amesema Mgumba.


Hata hivyo amesema mipaka iliyowekwa na rasilimali zilizopo kwenye ardhi ya mipaka hiyo zitabaki katika eneo husika kwa sababu wanaohudumiwa ni Watanzania, na mipaka hiyo inayowekwa ya kitongoji, kijiji, kata, tarafa, Wilaya na hata mkoa, haina maana yoyote kwa mwananchi wala kikwazo chochote kwa mwananchi yeyote.


"Hata mpaka ukiingia mwananchi yuko Kilindi na shamba au nyumba yake Iko Handeni, unarusiwa kwenda kulima au kuishi hukohuko Handeni, hii mipaka imewekwa kwa sababu yetu sisi tunaomsaidia Mh. Rais ili tupimwe kazi zetu zinaishia wapi, ndiyo maana yake" amefafanua.


Awali akifungua kikao hicho, mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Idrisa Mgaza amesema migogoro hiyo ni ya muda mrefu, hasa mipaka ya Mkoa wa Tanga kwa upande wa Wilaya ya Kilindi na Mkoa wa Manyara kwa upande wa Wilaya ya Kiteto.


Mgaza amebainisha kwamba wananchi walianza kupata nguvu ya kutatuliwa mgogoro huo baada ya kuona Waziri mkuu Majaliwa Kassim alikwenda kutembelea wilayani humo lakini baada ya muda kupita hapakuwa na kilichoendelea.


"Hivi karibuni alipoingilia Waziri Mkuu tukaona Ile kasi umeongezeka kutaka kutatua huu mgogoro lakini baadaye Ile kasi ikawa imepoa poa kidogo, na kwa hii kasi ambayo umekuja nayo wewe tuna amini unaweza kutatua huu mgogoro wa mpaka wa Kilindi na Kiteto" amesema Mgaza.


"Lakini kingine ni huu mgogoro uliozuka sasa kwa sisi wenyewe, kati yetu na Handeni, unatunyima usingizi kwa kweli, tulikuwa tunaoishi vizuri kama ndugu, lakini tukaona mambo yanabadilika kwa wenzetu, wamekuwa wakiingia katika maeneo yetu na kufanya mikutano ya hadhara na kuweka vikao,


"Pia wanajenga Mataasisi mbalimbali, tukiwauliza wanasema Kuna wananchi wao wamehamia huku hivyo wanakuja kutusaidia, sasa wanatusaidiaje bila sisi kufahamu, kwahiyo hili jambo limeleta mtafaruku mkubwa sana" amebainisha.

Post a Comment

0 Comments