Ticker

6/recent/ticker-posts

MMILIKI WA HOTELI MBARONI KWA KUJIUNGANISHIA MAJI KINYEMELA

Fundi bomba kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) Stephen Minja akifumua mfumo uliyounganishwa mmiliki wa hoteli ya Tema,Ebeneza Foya iliyopo mtaa wa Nyabulogoya mkoani Mwanza.
Meneja wa kitengo cha upotevu wa maji kanda ya Nyegezi,kutoka (MWAUWASA), Ramadhani Mramba akiwaonyesha waandishi wa habari bomba lililounganishwa kinyemela na mmiliki wa hoteli ya Tema, Ebeneza Foya kutoka wananchi na kupelekea changamoto ya maji kwenye mtaa wa nyabulogoya.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyabulogoya uliopo Kata ya Nyegezi wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, Renatus Mayanda amesema walipokea malalamiko ya changamoto ya maji kwa muda mrefu kutoka kwa baadhi ya wananchi wa eneo hilo baada ya kufatilia waligundu chanzo cha tatizo hilo.
Meneja wa kitengo cha upotevu wa maji kanda ya Nyegezi,kutoka (MWAUWASA), Ramadhani Mramba akiwaonyesha waandishi wa habari bomba lililounganishwa kinyemela na mmiliki wa hoteli ya Tema, Ebeneza Foya kutoka wananchi na kupelekea changamoto ya maji kwenye mtaa wa nyabulogoya.

****************

Na Sheila Katikula,Mwanza

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Mwanza (MWAUWASA) imemkamata Mmiliki wa hoteli ya Tema, Ebenezea Foya kwa kosa la kujiunganishia maji kiholela, kinyume na sheria, taratibu na kanuni za mamlaka hiyo hali iliyopelekea upotevu wa mapato ya serikali na wananchi kukosa huduma ya maji kwenye mtaa wa Nyabulogoya.

Akizungumza leo Meneja wa kitengo cha upotevu wa maji kanda ya nyegezi, Ramadhan Mramba wakati wa oparesheni iliyofanywa na Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wananchi wa eneo la Nyabulogoya lililopo wilayani Nyamagana, amesema baada ya kupata malalamiko kutoka kwa viongozi na kupelekea kutembelea eneo hilo na kubaini wizi wa maji.

Mramba ameeleza kuwa mmiliki wa hoteli hiyo alikatiwa maji mwaka mmoja uliopita kwa kudaiwa deni la maji na mamlaka hiyo.

"Mtuhumiwa alikatiwa maji baada ya hapo alijiunganishia bila kufanya jitihada zote za kurudishiwa maji pamoja na kufata taratibu zinazotakiwa kutoka mwauwasa" amesema Mramba.

"Inaonekana mmiliki huyo alijiunganishia maji kwa muda mrefu kwani kumekuwa na upotevu wa maji usiopungua lita 18 hadi 20 Kwa siku," amesema Mramba.

Naye Mkuu wa kanda Msaidizi upande wa mauzo, Stephen Otonde amesema mtuhumiwa huyo ni mteja wao amekuwa akitumia akaunti tatu za maji kwa majina matatu tofauti.

"Sisi kama Mwauwasa tulimkatia maji January 2020 -2021 kwenye akaunti tatu zote kwa sababu zilikuwa zinadaiwa huku kila akaunti ikiwa na jina lake.

Akaunti ya kwanza ni Jamal Awadh ikidaiwa sh 9,095,050, akaunti ya pili ni Ebenezea Foya inadaiwa sh 907467.86 na akaunti ya tatu ni John Foya ilikuwa ikidaiwa sh 78,499.

Mwanasheria wa serikali kutoka Mwauwasa, Oscar Twakazi ameeleza kuwa walipokea malalamiko kutoka kwa mwanachi ambaye ni mmoja wa wateja wao kuwa mmiliki wa hoteli ya Tema amejiunganishia maji kinyume na taratibu za Mwauwasa.

"Kiukweli ni kwamba mteja huyo alikuwa ni mmoja kati ya waliositishiwa huduma ya maji kutokana na kudaiwa," amesema Twakazi.

Amesema mmiliki wa Tema Hoteli alijiunganishia maji sehemu tatu ikiwemo kwenye hoteli,hosteli na kwenye nyumba jirani kwa kukata mabomba ya wananchi na kusababisha ya changamoto ya maji kwa wakazi wa eneo hilo kinyume na utaratibu wa sheria ya makosa ya jinai sheria namba (5) ya mwaka 2019.

Oscar amesema mmiliki huyo aliwahi kukamatwa kipindi cha nyuma akiwa amejiunganishia maji na waliweza kumfanyia maksio ya maji aliyotumia na kutozwa faini ya sh Milioni 1.5

Mwenyekiti wa mtaa wa Nyabulogoya, Renatus Mayanda amesema walipokea malalamiko muda mrefu kutoka kwa wananchi wa eneo hilo kuhusu tatizo la kukosekana kwa maji na kupelekea kukaa kikao na baraza la wazee la mtaa huo na kuazimia kufatilia kwa ukaribu na kumubaimi mmiliki wa hoteli hiyo.

"Tuliamua na baadhi ya wazee kuonana naye mmiliki wa hoteli hii lakini hatukufanikiwa kwani baraza liliamua kuniagiza niende moja kwa moja MWAUWASA kufikisha malalamiko hayo" amesema 

Jitihada za kumtafuta mmiliki wa hoteli hiyo zilifanyika kwa njia ya kumpigia simu lakini hakutoa ushirikiano ili kujibu mashitaka hayo.


Post a Comment

0 Comments