Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS YATOA WITO KWA WAZALISHAJI NA WAINGIZAJI WA MABATI NCHINI KUZINGATIA VIWANGO

Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Usimamizi wa Sheria TBS, Bw.Moses Mbambe akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12,2022 Jijini Dar es Salaam Afisa Viwango TBS, Bw. Arnold Mato akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12,2022 Jijini Dar es Salaam

*********************

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji na waingizaji wa mabati nchini kuhakikisha wanazingatia viwango ili kuzalisha mabati bora.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12,2022 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Usimamizi wa Sheria TBS, Bw.Moses Mbambe amesema bidhaa za mabati ambayo yanaingia nchini wamekuwa wakiyakagua kwa kuchukua sampuli na kupeleka maabara ili kujiridhisha na ubora wa viwango vya bidhaa hiyo.

Amesema wakibaini bidhaa hiyo haijakidhi viwango huchukua jukumu la kumtaka mwenye bidhaa arudishe bidhaa ilipotoka ama aiteketeze kwa kutumia gharama za mwenye bidhaa.

"Mwenye bidhaa anajukumu la kuiteketeza bidhaa yake ikiwa tumebaini haijakidhi viwango vya ubora, na kama tukijiridhisha inakidhi viwango basi, tunampatia cheti cha ubora na kumruhusu bidhaa zake kuingia sokoni". Amesema

Aidha amesema shirika la viwango huwa wanafanya ukaguzi katika soko kuhakikisha mabati yanayouzwa hapa nchini yanakidhi vigezo vya ubora kwa mujibu wa viwango husika, wanakwenda katika maghala ya waingizaji wa mabati pamoja na maduka yanayouza mabati kuchukua sampuli kwaajili ya kwenda kupima na wakibaini hayajakidhi viwango huchukua hatua stahiki.

Kwa upande wake Afisa Viwango TBS, Mhandisi Arnold Mato amesema matakwa ya viwango vya ubora wa bidhaa za mabati ni vipimo kama unene , urefu na upana ikiwa ni pamoja na migongo .

"Katika vipimo vya unene mara nyingi tunaangalia unene ambao unaanzia geji 30-32, 28,26, lakini bidhaa zote hizi mwisho ni geji 30 na kama kuna atakayezalisha geji zaidi ya 30 mfano 32 basi takwa la kiwango linamtaka mzalishaji huyo kuandika ili kumjulisha mteja kwamba bati hilo sio kwa matumizi ya kuhezekea".

Post a Comment

0 Comments