Ticker

6/recent/ticker-posts

WANANCHI MOA WALIA NA UVUVI HARAMU, WAIOMBA SERIKALI

Mgumba akisisitiza jambo kwa watumishi wa halmashauri.
Mgumba akiongea na wasimamizi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya.
Mgumba akipata maelezo ya mchoro wa ramani ya hospitali ya Wilaya.


*************************


Na Hamida Kamchalla, TANGA.


WANANCHI wanaoishi ukanda wa bahari ya Hindi katika kata ya Moa, Wilaya ya Mkinga wameiomba serikali kuwapa ushirikiano katika kukabiliana na uvuvi haramu wa kutumia baruti unaofanywa na wavuvi wa nchi jirani ya Kenya.


Wametoa wito huo mbele ya mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba alipotembelea soko la samaki lililopo kata hiyo huku wakisema suala la uvuvi haramu limekua kero kubwa ambayo inawasababishia wavuvi wenyeji kufika mbali kwenda kuvuoa lakini kukosa samaki.


Haruni Dongo amebainisha kwamba katika kusimamia rasilimali za serikali kwa upande wa bahari kuna kero nyingi ikiwamo hiyo ambayo inajitokeza mara nyingi na ili kudhibiti hali hiyo serikali haina budi kuingilia kati kwani wananchi peke yao hawawezi licha ya kuwepo kwa kikosi cha kudhibiti magendo cha KMKM cha Zanzibar.


"Na katika shuhuli zetu za usimamizi wa bahari bado tunasumbuliwa na suala la uvuvi haramu katika bahari yetu na wavuvi hao ni wenzetu wa nchi jirani ya Kenya, ingawa tuko kwenye suala la ujirani mwema lakini ni shida kubwa".


"Kilichopo sasa kwa wavuvi wetu wanakwenda kuvua mbali, mvuvi anatola alfajiri akirudi hapa anarudi na samaki kilo moja, hali ya bahari ni mbaya, uvuvi haramu umetawala katika maeneo yetu ya bahari, hivyo tunaiomba serikali ituunge mkono katika kupambana na hali hii" amesema Dongo.


Aidha wananchi hao wamelalamikia suala la mipaka ambayo hasa ndiyo inayosababisha wavuvi kutoka Kenya na kuingia nchini na endapo suala Hilo halitatafutiwa ufunbuzi hata maendeleo ya eneo hilo la uvuvi haliwezi kuendelea kimaendeleo hususani kwenye ujenzi wa soko kubwa la samaki.


"Muingiliano mkubwa wa wavuvi wa Kenya kuja kuathiri miamba yetu ambayo ndiyo mazalia makubwa ya samaki na ikizingatia wao kule upande wao hawana maeneo ya kuvuna wala hawana samaki kama wetu, suala la ujirani mwema lipo, ushauri wangu tu, iangaliwe namna ya kuliingilia kati hili" amesisitiza.


Akijibu kero wananchi hao, mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesema suala la uvuvi haramu, tunalichukua na tutaenda kulijadili katika vikao vyetu vya ulinzi na usalama mkoani kule, lakini pia tutaongea kwenye vikao vyetu vya ujirani mwema na wenzetu wa Kenya,


"Hatuwezi kukubali waje wachukue rasilimali zetu huku wakati sisi tupo, lakini pia niseme mmetukumbusha wajibu wetu, askari wetu wa kulinda mipaka" amesema.


Awali Mgumba amebainisha kwamba serikali imeandaa fedha kwa ajili ya wavuvi ambapo aliwataka kuunda vikundi ili wapatiwe mikopo ya boti za kisasa zitakazo wawezesha kufika mbali kwenda kuvuoa samaki wakubwa.


"Lengo la Mh. Rais ni kuwatoa watu wa Mkinga na kuwainua kiuchumi ili muwe na maisha bora zaidi, ombi lake kwenu, mjiunge kwenye vyama vya ushirika vya wavuvi, kwa sababu mzigo upo tayari" amesisitiza Mgumba.


Hata hivyo Mgumba amesisitiza kwa wananchi hao kuwa mbali na uvuvi wanapaswa pia kujikita na kujiimarisha katika kilimo cha korosho.


Katika ziara hiyo mbali na kuzungumza na wananchi pia Mgumba ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo hospitali ya Wilaya ya Mkinga, upanuzi wa mradi wa maji Parungu, kukagua zahanati ya kijiji cha Mayomboni.

Post a Comment

0 Comments