Ticker

6/recent/ticker-posts

WORLD VISION YAWEZESHA VIJANA KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Handeni Stephen Saitoti.

************************

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.


KATIKA kupambana na mabadiliko ya tabianchi, Shirika la World Vision nchini kupitia mradi wake wa mabadiliko ya tabianchi limewawezesha na kuwapatia mafunzo vijana katika kata tatu za halmashauri ya Wilaya ya Handeni.


Akiongelea manufaa yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo wilayani humo, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo Recho Mbelwa alisema vijana hao kwa sasa wana uzoefu wa kufanya kwa vitendo katika kulinda mazingira ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii.


Mbelwa amefafanua kwamba katika kuwaunga mkono vijana hao halmashauri imeshaanza kuwapatia mikopo ili waweze kuendelea kupambana na hali hiyo ambayo kwa Wilaya ya Handeni kwa sasa ina msukosuko wa uharibifu wa mazingira kutokana na watu kukata miti bila utaratibu.


"Kutokana na hali ya mabadiliko ya tabianchi, World Vision likiwa ni Shirika la Kiserikali limewezesha vijana katika ka za Kwamgwe, Segera na Kwedizinga, lakini kupitia mradi huu sisi halmashauri ya Wilaya tumeweza kutoa mikopo kwa vijana kwasababu moja ya matatizo kwa vijana ni masuala ya kiuchumi"


"Hawana fedha ya kutosha katika kutekeleza miradi yao ya kiuchumi, sasa ili waweze kutekeleza miradi hiyo tumewawezeaha kuwapa mikopo, katika kata ya Segera tumewezesha kikundi kimoja, Kwamgwe kimoja na Kwedizinga vikundi vitatu" amesema.


Aidha amesema katika kuwawezesha viana hao wapo ambao wamepatiwa vyerehani huku wengine wakiwa na vitalu vya miti ambavyo baada ya kuboresha wanagawa miti kwa wananchi ambao wana uhitaji kwa ajili ya kuboresha na kutunza mazingira.


"Wananchi wenye uhitaji ni wengi, kwani tayari vijana wameshaanza kugawa miti na hata wengine wanakuja kuichukua ikiwa bado haijafikia muda wa kutoelewa, tunawashukuru world vision, kwa kazi nzuri wanayoifanya na pia tutaendelea kuwahamasisha na kuwashirikisha vijana katika suala zima la utunzaji wa mazingira" amebainisha.


"Kuna vijana wa jamii ya wafugaji kule kata ya Misima, kijiji cha Msomera nao tutawahamasisha, wale wametokea katika maeneo ambayo walikuwa hawalimi wa kupanda miti, sasa huku wamekuja kwenye kilimo kwa hiyo wanahitajika kupewa elimu hii" amesema.


Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Handeni Stephen Saitoti amesema mradi huo umeweza kuwanufaisha wananchi wa Wilaya hiyo kwa takribani miaka mitatu huku alishurukuru Shirika hilo kwa kushirikiana na vizuri katika kupambana kutunza mazingira.


"Tunaishukuru sana world vision kwa kushirikiana na sisi kwa ukaribu, wameweza kutusaidia kufikia vijiji nane katika halmashauri yetu na kutengeneza vijana ambao mbali na shuhuli zao za kawaida wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu mabadiliko ya tabianchi" amesema.


"Mradi huu kwanza tumeyapokea na sasa tumeona una manufaa makubwa hasa kwa upande wa hawa vijana ambao wamewezeshwa elimu ya mabadiliko ya tabianchi wamekuwa na manufaa chanya katika jamii wanazoziishi" amebainisha.

Post a Comment

0 Comments