Ticker

6/recent/ticker-posts

BARABARA YA PANGANI KULETA CHACHU YA MAENDELEO MKOA WA TANGA.



*********************

Na Hamida Kamchalla, PANGANI.

MKUU wa Wilaya ya Pangani Ghaibu Lingo amesema tatizo kubwa lililokuwa likiikumba Wilaya hiyo ni barabara inayotoka Tanga mjini mpaka Bagamoyo ambapo kwasasa umetekelezwa kwa asilimia kubwa na kuleta manufaa makubwa.


Lingo amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo imetoa fedha za utekelezaji kwa wakati na kuwapa matumaini mapya wananchi kwakuwa wanatambua itakwenda kuwa chachu ya maendeleo Wilaya na Mkoa kwa ujumla.


"Sisi wananchi wa Pangani tumenyfaika kwa kiasi kikubwa sana hasa katika miradi ya maendeleo, tulikuwa na tatizo kubwa la barabara ya kutoka Tanga, Pangani, Kwamsisi, Makurunge hadi Bagamoyo ambalo hata ufumbuzi wake ulikuwa mkumu kupatikana"


"Barabara hizi sasa ziko katika hatua mbalimbali za kiutekelezaji, kutoka Tanga hadi Pangani ipo kwenye hatua ya umaliziaji wa kuumba umbo la barabara na kumwaga lami, lakini kutoka Pangani, Makurunge hadi Bagamoyo ipo kwenye hatua ya uchongwaji, hili ndilo lilikuwa tatizo kubwa la Wilaya yetu,


"Na sisi tunasema asante sana Rais wetu, hii barabara itakuwa sehemu ya chachu ya maendeleo ya nchi hii kwani tunaamini kwa kumalizika kwa barabara hizi nasi tutabadilika kimaendeleo" amefafanua Lingo.


Aidha amebainisha kuwa Wilaya hiyo Ina vijiji 32 ambavyo kwa sasa vyote viko kwenye utaratibu wa miradi ya umeme, ambapo 31 viko kwenye mradi wa umeme unaotumika huku viwili viko kwenye mradi wa kujenga umeme ambavyo ni Langoni na Uyuni.


"Kijiji cha Langoni nguzo zimesha simamishwa na wakandarasi wako kwenye hatua ya kutandaza waya lakini kijiji cha Uyuni nguzo zinapelekwa, kwahiyo vikikamilika hivyo itafanya Wilaya yetu vijiji vyote kuwa na umeme" amebainisha.


Lingo amefafanua kuhusu suala la miradi ya maji kwamba ndani ya kata zote 14 wilayani humo zina miradi ya maji yanayotoka lakini kuna tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwani maji hayo yana chumvi.


"Maji yapo na yanatoka, tuna tatizo kuwa na maji ya chumvi, lakini liko mbioni kutatuliwa kupitia mradi mkubwa wa maji kwa mto Pangani ambao na sisi tupo,


"Lakini kwa upande wa afya Rais kafanya vitu vikubwa sana, tumeletewa fedha za kutosha ambazo miradi yake kuna ambayo imeanza kutumika na mingine iko katika hatua za umaliziaji, kwahiyo utakuta sisi kihiduma za jamii tumekamilika" amesema Lingo.


Vilevile amesema kwa upande wa elimu, Wilaya imepata zaidi ya sh bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari kubwa ambazo zitasaidia kupunguza adha ya wanafunzi kutenbea mwendo mrefu lakini pia moja kati ya hizo itakuwa ni ya vipaji maalumu.


"Kwa ujumla utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilaya yetu inatekeleza kwa wakati na sasa maendeleo yetu yanakwenda kuimarika na uchumi kukua kwa kuongeza mapato yetu ya ndani" amefafanua Lingo.

Post a Comment

0 Comments