Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT.MPANGO AIPONGEZA TIMU YA WATAALAMU KUPUNGUZA KERO ZA MUUNGANO


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa Kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage,Treasury Square Jijini Dodoma leo tarehe 06 Desemba 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah wakishuhudia utiaji saini katika hati nne za makubaliano ya uondoaji hoja zilizopatiwa ufumbuzi kwenye orodha ya hoja za Muungano.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah wakiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage,Treasury Square Jijini Dodoma leo tarehe 06 Desemba 2022.

***********************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amepongeza timu ya watalaamu pamoja na wajumbe wa kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zilizofanyika kupunguza kero Nne kati ya Nane za Muungano zilizokuwa zimebaki tangu kufanyika kwa kikao hicho Agosti mwaka 2021.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifunga kikao cha kamati ya pamoja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika katika Ukumbi wa wa Kambarage,Treasury Square Jijini Dodoma leo tarehe 06 Desemba 2022.

Amesema Kamati hiyo ni chombo muhimu katika kukuza undugu, ushirikiano , biashara na uchumi pamoja na kukuza umoja na tamaduni za wananchi wa pande zote mbili za muungano.

Makamu wa Rais amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kujadili hoja zilizobaki kwa nia za kujenga na kuimarisha muungano kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi wajumbe wa kamati ya pamoja kuendelea na jitihada za kuongeza maarifa juu ya Muungano ikiwemo kusoma vitabu ili kuweza kuulinda na kuutetea vema muungano.

Hoja zilizopatiwa ufumbuzi katika kikao hicho ni pamoja na malalamiko ya Wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanapoagiza mizigo kutoka nje ya nchi na kupeleka Tanzania bara, hoja ya kodi ya mapato na kodi ya zuio, hoja ya ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO pamoja na hoja ya mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (Terminal III).

Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah, Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhandisi Zena Said , Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka pande zote za Muungano, Makatibu na Manaibu Makatibu wakuu, Wakuu wa taasisi mbalimbali pamoja na Sekretarieti ya Kamati ya pamoja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments