Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA MGENI RASMI MAONESHO YA KITAIFA YA YST 2022



Mwanzilishi Mwenza wa Young Scientists Tanzania (YST) Dkt.Gozibert Kamugisha akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 4,2022 Jijini Dar es Salaam kuelekea Maonesho ya YST yatakayofanyika Desemba 8,2022 kwenye hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam. 

Afisa Mtendaji wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation Bi.Caren Rowland akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 4,2022 Jijini Dar es Salaam kuelekea Maonesho ya YST yatakayofanyika Desemba 8,2022 kwenye hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam 

******************* 

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Kitaifa ya YST 2022 ambayo yamepangwa kufanyika Desemba 8,2022 Jijini Dar es Salaam. 

Kazi za kisayansi na teknolojia zitakazoonyeshwa kwenye maonesho hayo zimejikita zaidi katika masuala ya njia salama za utunzaji wa mazao ya kilimo,utunzaji wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali ya maji, dawa za asili na uboreshaji afya za binadamu, upatikanaji na uzalishaji wa nishati ya umeme, matumizi ya muziki katika ufundishaji wa somo hesabu mashuleni, matumizi ya mimea ya asili katika kuboresha uzalishaji wa maziwa ya ng'ombe na kutatua tatizo la udumavu wa ukuaji wa kuku. 

Hayo yamesemwa leo Desemba 4,2022 na Mwanzilishi Mwenza wa Young Scientists Tanzania (YST) Dkt.Gozibert Kamugisha wakatiakizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam. 

Amesema mwaka huu idadi ya wanafunzi waliowasilisha maombi ya kufanya kazi za ugunduzi imeongezeka kwa kiasi kikubwa hadi kufikia 1,143, kati ya idadi hiyo jumla ya kazi za utafiti na kisayansi 530 zimepatiwa usaidizi ambapo wanafunzi walioziandaa wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuziboresha na hatimaye kazi za kisayansi na ugunduzi 380 zimekamilika. 

Aidha Dkt.Kamugisha amesema mpango huu wa kuimarisha sayansi na ugunduzi kwa vijana unawezeshwa na wadhamini wakuu wa YST ambaoni Karimjee Jivanjee Foundation/Toyota Tanzania. 

"Tunatoa shukrani kwa wadhamini wetu wengine kama Shell Exploration and Production Tanzania Limited (Shell Tanzania), Institute of Physics, Speedy Print, Exim Bank Tanzania Ltd, Concern Worldwide na COSTECH". Amesema 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation Bi.Caren Rowland amesema wamekuwa wakitoa ufadhiri kwa wanafunzi ambao wamekuwa washindi wa YST, pindi wanapomaliza masomo yao ya elimu ya juu hivyo mpaka sasa wameshafadhiri wanafunzi 37 na watadhamini wanafunzi 4 kwa mwaka 2022 na wataendelea kuwa bega kwa bega na YST. 

"Wanafunzi ambao wameshapata udhamini wamekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuwa madaktari, wahandisi, wanasayansi na wameonesha mabadiliko makubwa hapa nchini". Ameeleza Bi.Caren.

Post a Comment

0 Comments