Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki amewataka walimu kote nchini Kufuata taratibu zilizoanishwa kwenye Waraka namba 24 wa mwaka 2002 ambao umeeleza wazi ni nani mwenye Mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko na viboko Vingapi vinaruhusiwa na kwa utaratibu upi vinatolewa kwa wanafunzi.
Waziri Kairuki ameyasema hayo Leo Januari 25,2023 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Viongozi wa Elimu ngazi ya Halmashauri kwenye kikao kazi cha uboreshaji wa Usimamizi wa Elimu Msingi na Sekondari Jiji la Dar es Salaam.
"Suala zima la adhabu ya Viboko mashuleni linaongozwa na Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002 na umeeleza bayana kabisa"
Waziri Kairuki ameendelea kufafanua kuwa Waraka huo na Kanuni za Elimu za mwaka 2002 lazima zifuatwe katika utolewaji wa adhabu ya viboko mashuleni.
"Kwa Mujibu wa mwongozo huo umeelekeza adhabu hiyo ya viboko inaweza kutolewa pale ambapo umetokea utovu wa nidhamu uliokithiri au makosa ya Jinai yaliyotendeka ndani au nje ya shule yenye muelekeo wa kuishushia heshima shule" amesisitiza Kairuki.
Pia Waziri ameendelea kuelekeza kuwa "kwa mujibu wa Waraka huo adhabu hiyo inavyotolewa lazima izingatie vigezo ikiwemo ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na haipaswi kuzidi viboko vinne kwa wakati mmoja"
‘Waraka huo umeeleza jinsi adhabu hiyo inapaswa kutolewa kwa mtoto Jinsia ya kike na kwa Mtoto Jinsia ya kiume. Kwa Mtoto Jinsia ya kike adhabu inapaswa kutolewa mikononi, na kwa mtoto Jinsia ya kiume ni kwenye Makalio. Pia Waraka huo umeeleza kuwa mwenye Mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko ni Mwalimu Mkuu au Mkuu wa shule husika au Mwalimu mwingine atakayekuwa ameteuliwa tena kwa maandishi.
Pia ametanabaisha kuwa kwa mtoto wa kike Imeelekezwa aadhibiwe na mwalimu wa kike au labda tu kama shule hiyo haina mwalimu wa kike ndipo anaweza kuadhibiwa na mwalimu wa kiume.
Waziri Kairuki ametoa rai kwa walimu wote nchini wakumbuke kuwa wamekasimiwa Mamlaka ya kuwa walinzi wa watoto wanapokuwa mashuleni kwa hiyo wasiwe sehemu ya kuwafanya watoto kuwa watoro kupitia adhabu wanazozitoa zinazokiuka taratibu, miongozo na Kanuni mbalimbali.
"Hatusemi watoto wasichapwe lakini wachapwe kwa kufuata taratibu na vigezo na kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa." amesisitiza Waziri Kairuki.
Pia ameonya Walimu wote Nchini watakaoendelea kukiuka Mwongozo huo kuwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa Sheria na Taratibu.
0 Comments