Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. KOMBA AMEWATAKA WASHIRIKI WA MAFUNZO KULETA MATOKEO CHANYA KWA WANAFUNZI.


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amewataka washiriki wa mafunzo endelevu ya walimu kazini wa Elimu ya Awali na Msingi ( Darasa la Kwanza na la Pili) kuzingatia mafunzo hayo ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi hao.

Dkt.Komba ameyasema hayo leo tarehe 2/2/2023 ikiwa ni siku ya kwanza ya mafunzo hayo.

"Tunatamani kuona gharama za mafunzo haya zinaendana na matokeo kwa wanafunzi, washiriki mnapaswa kutumia maarifa mtakayoyapata hapa katika kusimamia vizuri suala la kutojua kusoma na kuandika kwa wanafunzi.Tuzingatie na kuona umuhimu wa kuleta matokeo chanya kwa watoto" amesema Dkt.Komba.

Mafunzo hayo ya walimu kazini yameandaliwa na TET kwa kupitia Programu ya Serikali ya Shule Bora inayofadhiliwa na UKaid yana lengo la kuimarisha umahiri na weledi wa walimu katika utekelezaji wa Mitaala ya Elimu ya Awali na Msingi (Darasa la Kwanza na Pili) kwa kukuza stadi za Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu (KKK).

Washiriki kutoka Vyuo vya Ualimu, Maafisa Elimu Taaluma, Wakuza Mitaala na Walimu Mahiri wanashiriki mafunzo hayo kuanzia tarehe 2/2/2023 hadi tarehe 6/2/2023 na baadae washiriki hawa wanatarajiwa kwenda kuwezesha walimu wa madarasa ya awali, la I na la II. Aidha, viongozi wa elimu ngazi ya mkoa, wilaya, kata na shule watawezeshwa ili kuwajengea uelewa na uwezo wa kusimamia utekelezaji wake.

Mikoa sita (Dodoma, Mara, Pwani,Tanga,Simiyu na Rukwa) itahusika katika mafunzo hayo.

Post a Comment

0 Comments