Ticker

6/recent/ticker-posts

HOTELI YA HYATT REGENCY YAKABIDHIWA CHETI CHA HUDUMA SALAMA YA VYAKULA


Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora ( TBS) Lazaro Msasalaga(kulia) akikabidhi cheti cha huduma salama ya vyakula Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli ya Hyatt Regency Alexander Eversberg (kushoto)

*********************

SHIRIKA la Viwango Tanzania(TBS) wameikabidhi Cheti cha Utoaji huduma salama ya vyakula Hoteli ya Hyatt Regency ya jijini Dar es Salaam ambayo inakuwa Hoteli ya kwanza nchini kupata cheti hicho nchini.

Aidha TBS imetoa rai kwa wamiliki wa hoteli mbalimbali nchini kuhakikisha wanatambulika katika utoaji wa huduma bora kwa wateja wao ili kuvutia watalii wengi nchini na kukuza uchumi wa nchi pamoja na hoteli zao.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhi Cheti hicho kwa uongozi wa Hoteli ya Hyatt Regency, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS Lazaro Msasalaga amesema hoteli hiyo imekabidhiwa cheti hicho cha huduma salama ya vyakula baada ya kukidhi vigezo vilivyopo Kitaifa na Kimataifa.

"Hoteli hii ni ya kwanza nchini kutambulika kwenye utoaji wa huduma salama ya chakula kinachozingatia afya, kuwa na hoteli nyingi kutatufanya tuvutie zaidi watalii kuja hapa nchini kwa kuwa wanajua wakifika watapata huduma bora,"amesema.

Ameongeza kuwa katika uchumi Cheti hicho kitasaidia kuongeza watalii nchini Tanzania kwani watakuwa wakivutiwa na usalama wa vyakula watakavyokutana navyo katika hoteli lakini pia itasaidia kuongeza mapato yatokanayo na kodi kwa watalii wakija kwa wingi ,hoteli itapata fedha na kulipa kodi.

Msasalanga amesema, cheti hicho ni alama muhimu katika kuwavutia watalii kuona wanaweza kupata huduma bora ya chakula kilichofuata mifumo ya usimamizi wa ubora ambayo Ina viwango vya kimataifa.

Akizungumza kuhusu upatikanaji wa vyeti, Msasalaga amesema hoteli husika itapaswa kuandika barua kwa TBS ili wakafanye ufuatiliaje wa huduma kama zinazingatia kanuni za afya na pale mapungufu yanapobainika mtoa huduma husika hupewa mbinu namna ya kuboresha huduma.

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wamiliki hoteli kuhakikisha wanaingia kwenye mchakato huo wa hiyari ambao mwisho utawawezesha kupata cheti kama ambacho wamekipata Hayatt Regency.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa hoteli ya Hyatt Regency Alexander Eversberg amesema cheti hicho kitawaongezea wafanyakazi morali kwenye utendaji.

"Cheti hiki kitatuongezea ufanisi na hii itatufanya kuendelea ushirikiano wetu na TBS kwetu hii ni hatua nzuri"amesema huku wakijisifu kwamba wamekuwa wa kwanza kupata cheti hicho na kwamba wanaishukuru Serikali na TBS kwa kuwa bega kwa bega katika kufanikisha upatikanaji wa cheti hicho.

Wakati huo huo Ofisa Usalama wa hoteli hiyo David Oscar amesema wanayo furaha kupokea cheti hicho kutoka Shirika la Viwango Tanzania kwani hiyo ni ishara ya kwamba wamekidhi matakwa ya Sheria yanayowezesha kupata cheti hicho nacho wanajivunia nacho.

"Tumepata cheti hiki lakini maswali mengi yatakuwa cheti hiki kinatusaidia nini , cheti hiki kitaisadia kuhakikisha mfumo wetu wa chakula ni safi na Salama,naweza kusema sehemu nyingi wanatoa chakula lakini je chakula ni safi na Salama?

" Hivyo cheti ambacho tumekipata kinawahakikishia wateja Wetu na wote ambao wanakuja kupata ya huduma ya chakula kuwa na uhakika wa usalama wa chakula watakachokula."

Post a Comment

0 Comments