Ticker

6/recent/ticker-posts

NEMC YANG'ARA KIMATAIFA MAONESHO YA KILIMO NA MAZINGIRA QATAR


Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Baraza la Taifa la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Irene John akimkabidhi mfuko mbadala mmoja wa wageni waliotembelea banda la NEMC katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mazingira nchini Qatar na kupewa elimu jinsi Tanzania ilivyofanikiwa kutokomeza matumizi ya mifuko ya plastiki, pembeni ni maofisa wengine wa NEMC.


Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Baraza la Taifa la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Irene John akimuelezea mmoja wa wawekezaji waliotembelea banda la NEMC katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mazingira nchini Qatar namna NEMC lilivyorahisisha mazingira ya kusajili miradi kwa kufanya Tathimini ya Athari kwa Mazingira (TAM) hasa katika uwekezaji wa Kilimo, Mifugo na Viwanda.


Wageni mbalimbali waliotembelea banda la NEMC katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mazingira nchini Qatar wakipata elimu ya namna NEMC lilivyorahisisha mazingira ya kusajili miradi kwa kufanya Tathimini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na utokomezaji mifuko ya plastiki.



Na Mwandishi Wetu, DOHA



Tanzania ni miongoni mwa nchi 130 zinazoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mazingira(Agriteq Expro 2023) ambayo hufanyika kila mwaka na kwa mwaka huu yanafanyika kuanzia tarehe 15 hadi 19 Machi, 2023 katika jiji la Doha nchini Qatar huku Baraza la Taifa la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) likionesha uzoefu wake kwenye masuala mbalimbali ikiwamo utokomezaji wa mifuko ya plastiki.

Katika maonesho hayo yaliyofunguliwa na Waziri wa Manispaa, Dk. Abdullah bin Abdulaziz bin Turki Al Subaie na yamejumuisha kampuni za kimataifa zaidi ya 300, wakulima zaidi ya 100 pamoja na wadau wa mazingira huku NEMC ikiwa miongoni mwa taasisi 16 zilizoshiriki kutoka Tanzania.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa NEMC, Irene John alisema maonesho hayo yatafungua fursa nyingi za uwekezaji katika bidhaa na huduma kupitia mawasilisho yaliyofanywa na NEMC imeonesha jinsi gani mazingira ya uwekezaji yameboreshwa kupitia mifumo mbalimbali ya kielektroniki kama vile mchakato wa utoaji vibali vya Tathimini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na pia mfumo wa upatikanaji wa vibali vya taka hatarishi ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji.


“Miongoni mwa wageni waliotembelea banda la NEMC ni pamoja na watumishi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, Wizara na kampuni mbalimbali kutoka nchi washiriki, mwananchi mmoja mmoja kutoka Qatar na nchi mbalimbali walitembelea banda la NEMC ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa aina mbalimbali ili kupata elimu pamoja na kuelezwa fursa za uwekezaji kwenye mazingira, utalii na kilimo,”alisema.



Kadhalika, Ofisa Mazingira kutoka NEMC Kanda ya Kusini, Obasanjo Nniwako alieleza kuwa moja ya faida kubwa kwa NEMC kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya mazingira na kilimo ni pamoja na kuitangaza NEMC na pia kutoa elimu juu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa uwekezaji endelevu.



“Lakini pia tumeeleza jinsi Tanzania ilivyotokomeza matumizi ya mifuko ya Plastiki na kuonesha kwa vitendo baadhi ya mifuko mbadala inayotumika ambayo ni rafiki kwa Mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,”alisema.



Naye, Tilisa Mwambungo Afisa Mazingira toka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, aliongeza kuwa kwenye maonesho wanatangaza fursa zilizopo za uwekezaji hasa katika kilimo endelevu kinachozingatia uhifadhi wa mazingira pamoja na utalii kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira.





“Kwa ujumla wake, maonesho yametoa fursa kwa washiriki kutoka Tanzania kueleza Mataifa juu ya maeneo mbalimbali ya uwekezaji nchini Tanzania, hususani katika sekta ya kilimo, ufugaji, utalii na madini ambazo zinapatikana nchini Tanzania na NEMC imeweza kutoa elimu kwa washiriki waliotembelea banda letu kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa wakati wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuwekeza nchini Tanzania,”alisema.



Maonesho hayo yanalenga kutoa fursa kwa washiriki kuonesha bidhaa na huduma zinazohusiana na kilimo na mazingira, kubadilishana uzoefu, teknolojia pamoja kutafuta masoko na fursa na uwekezaji katika kilimo kinachozingatia uhifadhi wa mazingira.



Mbali na NEMC, washiriki wengine kutoka nchini Tanzania ni pamoja na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania -Qatar, Wizara ya Kilimo, Bodi ya Mkonge, Mama Afrika, SL. Afrika, Dumas Afrikan Market, Msai Sandals, Habimaya Solutions, Natural Shine Trader, Nkona Limited, Linga Enterprises, MamboJambo Design, Kolumba Art Studio, Afnaan Limted pamoja na Amahoro Afrika Limited.



Mwisho.

Post a Comment

0 Comments