Ticker

6/recent/ticker-posts

BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU IMEZINGATIA VIPAOMBELE MUHIMU KATIKA MASUALA YOTE YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI



Na.Mwandishi Wetu - Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu imezingatia vipaombele muhimu katika maeneo yote yanayoratibiwa na Ofisi hiyo ili kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija kwa Taifa.

Ametoa kauli hiyo mapema leo wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Mwaka wa fedha 2023/24 leo Aprili 13, 2023 wakati wa Kikao cha Bunge la 12 Mkutano wa 11 Kikao cha sita Mjini Dodoma.

Waziri Mhagama amesema pamoja na mambo mengine, Bajeti ya Mwaka huu ya Ofisi ya Waziri Mkuu imezingatia masuala muhimu ikiwemo la Uratibu wa shughuli za Serikali kwa kueleza tayari ofisi hiyo umeunda Idara ya ufuatiliaji na Tathimini ya utendaji wa serikaliambapo itawezesha kuwa na taarifa sahihi za utekelezaji wa Shughuki za Serikali.

Akizungumzia kuhusu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Waziri Mhagama amesema, Mamlaka imefanya kazi ya kutosha katika maeneo yote manne ya kimkakati ya kupambana na dawa za kulevya, kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya, kufanya ukaguzi katika maeneo yanayofanya biashara ya kemikali bashirifu na kufanya maboresho ya sheria na kuteketeza mashamba mengi ya bangi nchini.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Mamlaka imefanya vizuri katika kutoa elimu ya uelewa kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya.

“Tumefanya vizuri katika kupunguza athari za madhara ya dawa za kulevya kwa waathirika, na huduma ya za kutibu urahibu wa dawa za kulevya na bado tunaendelea kufanya mashirikiano ya nchi, kikanda na kimataifa ili kukabiliana na jambo hili mtambuka.”Alisisitiza

Kwa Upande wa suala la Sera ya lishe, Waziri amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, itakuja na Mkakati wa kuwa na Sera ya lishe, UKIMWI na Janga la matumizi ya Dawa za kulevya.

Pamoja na hilo, Waziri alieleza kuwa ofisi yale inasimamia Dawati la Afya Moja linaloshughulikia uratibu wa magonjwa ya mlipuko yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, ili kuweza kukabiliana nayo na kuangalia usalama wa wananchi.

Aidha alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kwa falsafa yake ya kuliwezesha Taifa kuwa na ustahimilivu na kuleta mabadiliko makubwa ya kiuongozi, kidemokrasia, kiuchumi na mahusiano ya kimataifa na kuwataka wabunge kuunga mkono falsafa hiyo.

Post a Comment

0 Comments