Ticker

6/recent/ticker-posts

ITUMIENI KAMPENI YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA - MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuitumia kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu, au vikundi vya watu ambao ama wanajihusisha na ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto.

Ametoa wito huo leo Alhamisi (Aprili 27, 2023) alipozindua kampeni hiyo ambayo itatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia Machi, 2023 hadi Desemba 2025.

Amesema kuwa kampeni hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji haki, mifumo ya utoaji haki, masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na taasisi za serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi.

“Kampeni hii pia itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa”. Amesema

Ameongeza kuwa, faida nyingine ya kampeni hiyo ni kusaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi zote yaani kuanzia Serikali kuu hadi Serikali za Mitaa. “Ushiriki wa wadau wanaojihusisha na huduma ya msaada wa kisheria utaongezeka kwa asilimia 80 katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria iweke mfumo mzuri wa kushughulikia changamoto za kisheria zitakazoibuliwa wakati wa Kampeni katika utimilifu wake. “Tusiache wananchi wakiwa bado hawajapata majibu ya changamoto zao. Hii itasaidia kujenga taswira nzuri kwa Serikali wala kwa mamlaka ambayo imeridhia kuwepo kwa Kampeni hii”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara hiyo itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa ili Watanzania wote waweze kuifikia haki na kuipata haki kwa wakati.

“Kwa wale ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili wa kujitegemea hakikisheni wanapata huduma za kisheria bila ya upendeleo wowote na kwa viwango stahiki”.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa kampeni hiyo ambayo ni maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanatoa elimu ya sheria na kusaidia wahitaji ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, wamepanga kutoa elimu katika maeneo ya migogoro ya Ardhi, mirathi, ndoa, sheria ya mtoto katika maeneo ya Ukatili wa kijinsia na Maadili

Amesema kuwa kampeni hiyo itatekelezwa pande zote mbili za Muungano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali na wasio wa serikali ikiwemo Ofisi ya Mashtaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ustawi wa Jamii, vyuo vya elimu ya juu,

Wengine ni CHAMA cha Wanasheria nchini (TLS), Mtandao wa Mashirika yanayotoa huduma ya msaada wa kisheria – (TANLAP), Taasisi ya Huduma za Kisheria (LSF), LHRC, EU, UNDP, WILDAF na Benki ya NMB

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Aprili 27, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimina na Waziri wa Katiba na Sheria , Dr. Damas Ndumbaro na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuzindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), Aprili 27, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa akizungumza na viongozi na wananchama wa Tanganyika Law Society wakati alipotembelea banda lao kabla ya kuzindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Aprili 27, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) ofisi ya Dodoma, Neema Ahmed (kushoto) wakati alipotembelea banda la maonesho la chama hicho kabla ya kuzindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Aprili 27, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Post a Comment

0 Comments