Ticker

6/recent/ticker-posts

JESHI LA POLISI SHINYANGA LAHAMASISHA AMANI SIKUKUU YA EID EL FITR

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewataka wananchi kusherehekea Sikukuu ya Eid El Fitri kwa amani na utulivu huku likiwaasa wazazi kutowaruhusu watoto wao kwenda kwenye kumbi za starehe kwani kumbi hizo zipo kwa ajili ya watu wazima na si watoto.


Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa Aprili 20,2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amewataka wananchi kusherehekea Sikukuu ya Eid El Fitr kwa amani na utulivu huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi kuwa hali ya utulivu mkoani Shinyanga ni endelevu.



Amesema Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawahakikishia wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuwa tutaendelea kuhakikisha kwamba hali hii ya utulivu iliyopo hivi sasa itakuwa ni endelevu kwa kipindi chote cha sikukuu ya Eid El Fitri na hata baada ya sikukuu.


"Tunaendelea kuwatahadharisha wazazi na wenye kumbi mbalimbali za starehe kwamba Disco toto ni marufuku. Kumbi yoyote itakayokutwa ikichezesha Disco toto itafungwa kwa kipindi chote cha sikukuu kwani Disco toto ni hatari kwa usalama wa watoto", amesema Kamanda Magomi.


"Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linapenda kuwataarifu wananchi wa mkoa wa Shinyanga kwamba kwa kipindi cha msimu wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hali ya usalama katika mkoa wa Shinyanga ilikuwa shwari kwani tangu kuanza kwa mfungo wa Ramadhani hadi hivi sasa, hakuna tukio kubwa lililojitokeza ambalo limehatarisha au kuleta taharuki katika jamii", ameongeza Kamanda Magomi.


"Nawatakia kila la kheri waislamu wote na wana Shinyanga kwa ujumla katika kusherehekea sikukuu ya Eid El Fitr. Lakini pia napenda kutoa wito kwa madereva wa Magari, Bodaboda, Baiskeli na watembea kwa miguu kuwa makini wawapo barabarani ili kuweza kuepuka ajali ambazo zinaweza kuepukika", amesema Kamanda Magomi.

Post a Comment

0 Comments