Ticker

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU KENYA: TANZANIA IPO MBALI KATIKA USIMAMIZI WA USALAMA NA AFYA


Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii Nchini Kenya, Mhe. Geofrey Kaituko akizungumza na baadhi ya viongozi wa OSHA na watumishi wa Wizara yake alioambatana (hawapo pichani) walipotembelea Ofisi za OSHA Dar es salaam kwa lengo la kujifunza jinsi Tanzania ilivyoweza kuwa na Taasisi inayojitegemea kwa ajili ya kusimamia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Adam Katundu, akimkabidhi zawadi Mtendaji Mkuu wa Idara ya OSHA Nchini Kenya, Dkt. Musa Nyandusi wakati wa ziara yao ya kutembelea ofisi za OSHA Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii kutoka Kenya pamoja na baadhi ya viongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa ziara ya viongozi hao kutoka Kenya ambao walitembelea Ofisi za OSHA Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza namna OSHA inavyosimamia usalama na afya mahali pa kazi nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu, na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii nchini Kenya, Mhe. Geofrey Kaituko (waliokaa) wakikwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Menejimenti ya OSHA na viongozi wa Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii nchini Kenya.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu (wapili kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii Nchini Kenya, Mhe. Geofrey Kaituko (wapili kulia) wakifualia mada mbali mbali kuhusu masuala ya kazi nchini. Wakwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya OSHA Nchini Kenya na wakwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.

********************

Na Mwandishi Wetu

Ujumbe wa Wataalam kutoka Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii kutoka Kenya umehitimisha ziara yake ya siku nne nchini iliyolenga kubadilishana uzoefu kuhusu sheria na taratibu mbali mbali za kazi ambapo wamesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa masuala ya kazi hususan mifumo ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi.

Akiongea mara baada ya kuhitimisha ziara yao katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi ya Kenya, Bw. Geoffrey Kaituko, amesema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitafuta uzoefu wa mambo mbali mbali ughaibuni ilihali uzoefu huo unapatikana katika nchi zinazowazunguka.

“Ziara yetu hapa Tanzania imekuwa ya kufana sana, tumetembelea Taasisi mbali mbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kwahiyo sisi tumefurahi sana kwa mapokezi mazuri tuliyoyapata pamoja na mambo mazuri tuliyojifunza. Mara nyingi tumekuwa na mazoea ya kwenda Ulaya kujifunza mambo fulani fulani mfano kwa mambo haya ya OSHA tungetaka kwenda Ujerumani wakati hapa Tanzania kuna Taasisi nzuri sana inayosimamia masuala ya usalama na afya hivyo jambo ambalo tunatoka nalo hapa ni kwamba nasisi ni lazima twende tukaanzishe Taasisi kama hii,” amesema Bw. Geoffrey Kaituko.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu, amesema kupitia ziara hiyo ya wataalam kutoka Kenya, Ofisi yake imejifunza mambo mengi ikiwemo jinsi walivyofanikiwa kuwezesha watu wao kupata ajira nje ya nchi yao na hivyo kuliingizia Taifa lao fedha nyingi za kigeni.

“Mfano katika suala la Wakenya wanaofanya kazi nje yan chi yao, Saudi Arabia wana wafanyakazi zaidi ya 120,0000, Qatar zaidi ya wafanyakazi 60,000 na nchi nyingine za Kiarabu zaidi ya 40,000 hivyo nimejifunza kwamba fedha wanayopata kutoka nje kutokana na ajira za nje ni zaidi hata ya fedha zinazotokana na mazao yao makuu ya biashara kama vile Kahawa na Chai. Nimemwelekeza Mkurugenzi anayehusika na Huduma za Ajira aangalie ni kwa jinsi gani tunaweza kujifunza kutoka kwa wenzetu ili nasi tuweze kunufaika na ajira za nje ya nchi,” ameeleza Prof. Katundu.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema ziara hiyo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano hususan kwenye eneo la sheria na taratibu mbali mbali za kazi baina ya OSHA Tanzania na Kenya jambo ambalo litakuza uwekezaji baina ya nchi zote mbili pamoja na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa sera ya soko la pamoja la Afrika Mashariki.

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri sana, tumejifunza kutoka kwao na wamejifunza kutoka kwetu lakini tunafahamu kuwa sisi ni Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika Jumuiya hii kuna kitu kinaitwa Soko la Pamoja (Common Market) na kuna wawekezaji wa Tanzania huko Kenya na wao wapo hapa kwetu. Hivyo ni muhimu sana kwa nchi hizi kuwa na ulinganifu wa sheria mbali mbali ili kuwezesha uwekezaji na biashara kufanyika katika mazingira mazuri,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Usalama na Afya katika Wizara ya Kazi Nchini Kenya, Dkt. Musa Nyandusi, amesema wapo mbioni kuunda Taasisi Mahsusi kwa ajili ya kusimamia masuala ya Usalama na Afya nchini kwao ili kuendana na miongozo ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) hivyo wanatarajia kujifunza mengi kutoka Tanzania ambayo imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa masuala husika.

Taasisi ya OSHA ilianzishwa rasmi Agosti 31, 2001 ikiwa ni jitihada za serikali ya Tanzania ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia pamoja na kukidhi matakwa ya Mikataba ya Kimataifa ya ILO inayozitaka nchi wanachama kuwa na chombo mahsusi cha kusimamia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Post a Comment

0 Comments