Ticker

6/recent/ticker-posts

MFUMO WA GePG WAONGEZA USALAMA WA MAPATO VYUONI

Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Usalama wa makusanyo ya mapato ya Vyuo Vikuu na vya Kati umeongezeka kwa kiwango kikubwa baada ya kuanza kutumika kwa mfumo wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG).

Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo (taaluma) kutoka Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Dkt. Momole Kasambala, wakati wa maadhimisho ya wiki ya Ubunifu yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Dkt. Kasambala alisema kuwa Mfumo wa GePG umerahisisha taasisi za elimu kukusanya maduhuli kwa ufanisi na kuwawezesha wanafunzi kufanya malipo mbalimbali yakiwemo ya ada kwa urahisi.

“Kupitia Mfumo wa GePG, mapato ya taasisi za elimu yanaongezeka na ni salama kupitia mfumo huo tofauti na hapo awali ambapo malipo yalikuwa yakifanyika kwa mlipaji kuonana ana kwa ana na mpokeaji wa fedha jambo lililokuwa likitoa mwanya wa upotevu wa fedha za taasisi.

Kwa upande wake Mbunge wa Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage, alisema kuwa Mfumo wa GePG unajieleza wenyewe kwa takwimu kwa kuwa unatoa namba ya malipo (Control Number) ambayo mtu anaweza kuitumia kufanya malipo eneo lolote hivyo kurahisisha ulipaji wa Mapato ya Serikali.

Aidha alisema kuwa, kwa kuwa mfumo huo unaonesha mapato yanayoingia, unasaidia Wizara ya Fedha na Mipango kuweka mipango mizuri kwa kujua mapato mengi yanapatikana mwezi gani na eneo gani na pia unasaidia viongozi katika kufanya maamuzi kwa kuwa muda wowote wanaona mapato yanayoingia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akisikiliza maelezo ya Mtaalamu wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Maendaenda, kuhusu matumizi ya Mfumo ya GePG kupitia simu ya mkononi, wakati wa maadhimisho ya wiki ya Ubunifu yanayofanyika kitaifa Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage, akisikiliza maelezo ya Mtaalamu wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Maendaenda, kuhusu matumizi ya Mfumo ya GePG kupitia simu ya mkononi, wakati wa maadhimisho ya wiki ya Ubunifu yanayofanyika kitaifa uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Bw. Edmundi Nzowa, akiuliza jambo kwa wataalamu wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Maendaenda (wa pili kushoto) na Stella Nguma, wakati wa maadhimisho ya wiki ya Ubunifu yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Mtaalamu wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Maendaenda (wa pili kushoto) na Stella Nguma, wakitoa elimu namna ya kutumia Mfumo wa GePG katika kupata huduma zikiwemo za kujaza taarifa za upotevu wa mali kwa kutumia mfumo huo, wakati wa maadhimisho ya wiki ya Ubunifu yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Mtaalamu wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Maendaenda (katikati) akitoa elimu kwa mkazi wa Mbarali, Mkoani Mbeya, Bi. Eva Lusanda, alipotembelea banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, wakati wa maadhimisho ya wiki ya Ubunifu yanayofanyika kitaifa jijini hapo.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)

Post a Comment

0 Comments