Ticker

6/recent/ticker-posts

RUWASA MKOA WA MTWARA KUTUMIA BILIONI 17 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI

Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cecil Mwambe akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namalombe mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji .

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Masasi Juma Yahaya akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji kijiji cha Namalombe wilayani humo.

Meneja wa Ruwasa mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damas wa kwanza kushoto na baadhi ya watumishi wa Ruwasa wakisubiri Mwenge wa Uhuru katika mradi wa maji Namalombe.

Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 lililojengwa katika kijiji cha Namalombe wilayani Masasi likiwa limekamilika.


****************************
Na Muhidin Amri,

Mtwara

WIZARA ya maji kupitia wakala wa
maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imepanga kutumia zaidi ya Sh.bilioni 17 kwa ajili ya ujenzi wa miradi 66 ya maji mkoani Mtwara.

Meneja wa Ruwasa mkoani hapa Mhandisi Primy Damas amesema kati ya miradi hiyo 34 ya kukamilisha na miradi 32 ni mipya na imeanza kutekelezwa katika wilaya zote za mkoa huo ili kuwaondolea wananchi kero ya huduma ya maji.

Damas amesema,kazi zilizopangwa kufanyika ni utafutaji wa vyanzo,kuchimba visima katika vijiji 24 na kufanya usanifu wa miradi katika vijiji 175.

Aidha ameeleza kuwa,hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu Ruwasa mkoa wa Mtwara imetekeleza jumla ya miradi 34 yenye thamani ya Sh.bilioni 25,063,484,536.44 katika vijiji 144.

Ametaja idadi ya miradi kwa kila wilaya ni Masasi yenye miradi 5 itakayonufaisha wakazi wa vijiji 16,Mtwara(10)kwa ajili ya vijiji 33,Nanyumbu 4 vijiji 5,Newala miradi 12 kwa vijiji 53 na Tandahimba iliyopata miradi 3 itakayowanufaisha wakazi wa vijiji 37.

Amesema,miradi mipya 32 imepangwa kujengwa katika maeneo mbalimbali na itakapo kamilika itatoa huduma kwa vijiji 141 na kwa sasa wako katika hatua mbalimbali za manunuzi.

Pia Damas ameeleza kuwa,Ruwasa ina mikakati mikubwa ya kuboresha huduma ya maji mkoani humo ikiwemo kutekeleza mradi wa kutoa maji mto Ruvuma hadi mji wa Mangaka ambao umetengewa jumla ya Sh.bilioni 38,230,921,377.06.

Kwa mujibu wake,Mkataba wa mradi huo umeshasainiwa na tayari mkandarasi kampuni ya AFCONS Ltd amekabidhiwa eneo la mradi na ameanza kazi chini ya mtaalam mshauri kampuni ya WAPCOS LTD.

Amesema, muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 20 kuanzia mwezi Julai 2022 na utakapokamilika utaweza kuhudumia zaidi ya wakazi 81,330 katika viunga vya mji wa Mangaka na vijiji vilivyopo pembezoni mwa bomba kuu.

Damas amevitaja vijiji vitakavyonufika ni Masuguru,Lukula,Chungu,Nanyumbu,Maneme,Namasoga,Chipuputa,Namaguruvi,Nakatete,Mpwahia,Mkohora,Nahawara,Makanya,Chitowe na Nanderu.

Hata hivyo amesema,sekta ya maji katika mkoa wa Mtwara inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji, kutopatikana kwa vyanzo vya maji vya uhakika hasa katika wilaya ya Nanyumbu na uchangiaji duni wa wananchi katika huduma wanayoipata ili kuifanya miradi iweze kujiendesha yenyewe na kuwa endelevu.

Amesema,katika kukabiliana na changamoto hizi wamejipanga kushirikiana na wataalamu wa Bonde la mto Ruvuma na Pwani ya kusini kutafuta vyanzo vya uhakika na kuendelea kuhamasisha wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kulipia huduma za maji.

Naye Meneja wa Ruwasa Wilayani Masasi Mhandisi Juma Yahaya alisema, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Ruwasa wilaya ya Masasi inatekeleza jumla ya miradi minane yenye jumla ya thamani ya Sh.bilioni 6.5 ambayo iko hatua mbalimbali za utekelezaji wake.

Alisema,miradi hiyo itakapokamilika itasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Masasi kutoka asilimia 73 hadi kufikia asilimia 80.

Post a Comment

0 Comments