Ticker

6/recent/ticker-posts

WAFUGAJI WA SAMAKI AINA YA SATO MKOANI RUVUMA, WAFURAHIA KUPATA SOKO LA UHAKIKA

Baadhi ya wafugaji samaki katika Mabwawa ya Msindo Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma wakiandaa samaki kabla ya kupeleka kwa wateja wao.
Mfugaji wa samaki Christopher Ndunguru akiwa na samaki aina ya Sato baada ya kuwavua kutoka kati ya mabwawa yake yaliyopo kijiji cha Msindo wilayani Newala.
Moja kati ya Bwawa la kufugia Samaki linalomilikiwa na Bwana Christopher Ndunguru.


***************

Na Muhidin Amri, Namtumbo

BAADHI ya wafugaji wa samaki katika mabwawa ya Msindo Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma,wameonesha kufurahishwa na uwepo wa soko la uhakika la samaki aina ya Sato walioanza kuzalishwa kwa wingi mkoani Ruvuma.

Wamesema,uwepo wa soko la uhakika wa kitoweo hicho umehamasisha sana kuongeza mabwawa kwa ajili ya ufugaji ili kujiongezea kipato na kuwawezesha kuishi maisha yenye nafuu.

Mmoja wa wafugaji hao Christopher Ndunguru amesema,ufugaji wa samaki unalipa sana kutokana na kuwa na faida kubwa licha ya kukutana na changamoto mbalimbali.

Alisema,toka vifaranga vya samaki wanapowekwa kwenye bwawa kwa mara ya kwanza ni hadi kuanza kuuza inachukua takribani muda wa miezi sita na katika kilo moja wanakaa samaki wawili au watatu na bei kwa kilo moja ni 10,000.

Ndunguru alisema,soko la samaki katika Manispaa ya Songea ni kubwa na la uhakika iwapo mfugaji atafuata kanuni za ufugaji wa kisasa atapata faida kubwa na kuondokana na changamoto mbalimbali za maisha.

Hata hivyo alitaja changamoto katika ufugaji wa samaki ni upatikanaji wa chakula kizuri ili kuwafanya samaki kukua haraka na mbegu sahihi aina ya Sato wanaopendwa sana na wakazi wa Songea na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Alisema,kwa sasa mbegu za samaki zinapatikana katika kituo cha serikali cha Luhira Manispaa ya Songea,Dar es slaam na mkoa jirani wa Mbeya,ambapo ameishauri serikali kuanzisha vituo vingi zaidi ya kuzalisha vifaranga vya samaki ili wananchi wengi waanze biashara hiyo.

Alisema,siku za nyuma walikutana na changamoto nyingi,lakini baada ya kuzibaini na kuzipatia majibu kwa sasa wanafuga kwa ufanisi na wameanza kupata faida na kunufaika na shughuli za ufugaji wa samaki.

“Ufugaji wa samaki kwa ujumla wake unalipa sana,kwa mfano sisi kwa sasa tumefika mahali samaki tunapowaweka kwenye bwawa hadi kuuza ni miezi sita,na bei yake Songea ni elfu kumi,hivyo ukiwa na kilo 100 unapepeleka sokoni baada ya muda mfupi unapata fedha yako yote,ufugaji wa samaki ni biashara nzuri sana”alisema.

Ametoa wito kwa watumishi wa umma, kuanza kuandaa shughuli nyingine ya kufanya wakiwa bado kazini badala ya kutafuta shughuli baada ya kuondoka katika utumishi kwani inaweza kuwaathiri kwa kukosa uzoefu.

Ditram Komba alisema, shughuli ya ufugaji wa samaki ni nzuri na ina faida kubwa na tangu alipoanza ufugaji wa samaki amepata mafanikio makubwa katika maisha yao
.
Ditram Damian,ameiomba serikali kupitia wizara ya mifugo na uvivu,kuweka mpango wa upatikanaji wa chakula bora cha samaki kitakacho tengenezwa hapa nchini badala ya kuagizwa nje ya nchi kwa kutumia mawakala kwa gharama kubwa.

Post a Comment

0 Comments