Ticker

6/recent/ticker-posts

WATOA HUDUMA ZA KIPOSTA WAASWA KUZINGATIA SHERIANa Mwandishi Wetu


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaasa watoa huduma za Posta nchini kuzingatia sheria, kanuni na miongozo wanapowahudumia wananchi kwa kusafirisha vifurushi na vipeto vyao kwenda maeneo mbalimbali. Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 imepewa jukumu la kusimamia sekta ya Mawasiliano na Posta.

Akizungumza kwenye Mkutano na wadau wa usafirishaji vifurushi na vipeto wapatao 70 uliofanyika jijini Dar es salaam, Afisa Mwandamizi wa Kitengo cha Huduma za Posta wa Mamlaka hiyo Joseph Zebedayo alisisitiza kuwa ni muhimu watoa huduma za kiposta kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na masharti ya leseni ili kuwapa wananchi huduma zenye viwango na vinavyotoa uhakika wa huduma.

“Tumekutana na wadau hawa ili kuwaelimisha kuhusu huduma wanazotoa na lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri za usafirishaji wa vifurushi na vipeto ukizingatia huduma hizi ni muhimu katika kuleta Maendeleo yetu,” alibainisha.

Mamlaka hiyo imekutana na wadau hao pembezoni mwa kampeni ya Elimu kwa umma inayotekelezwa kote nchini iitwayo “Tuma Chap kwa Usalama” ikilenga kuwahamasisha watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto nchini kuhakikisha wanasajili huduma zao kwa kupata leseni ya TCRA na wananchi kuhakikisha wakati wote wanapotumia huduma za usafirishaji vifurushi na vipeto wanatumia watoa huduma waliosajiliwa.

Pembezoni mwa Mkutano huo Afisa Mawasiliano Mwandamizi Mkuu Semu Mwakyanjala alibainisha kuwa TCRA inaendesha Elimu kwa umma iitwayo Tuma Chap, Kwa Usalama inayolenga kuwapa wananchi Elimu ya usafirishaji vipeto na vifurushi ili kuongeza tija ya mchango wa sekta ya posta kwenye uchumi.

“Mamlaka tunawakumbusha wananchi kuzingatia kutuma vifurushi na vipeto kwa mtoa huduma aliesajiliwa na watoa huduma kupata leseni ya TCRA ili kutoa huduma za kusafirisha Bidhaa za kiposta yaani vipeto na vifurushi, pia wale ambao leseni za kutoa huduma zimefikia ukomo tunawaasa wahuishe leseni hizo, kwani kutoa huduma za kiposta bila leseni ni kwenda kinyume na sheria,” alibainisha.

Mamlaka hiyo aidha ilionya kuwa watoa huduma wanaosafirisha vipeto na vifurushi wasiosajiliwa watambue kwamba kufanya huduma bila usajili ni kutenda kinyume na sheria. Huku ikiwataka kuzingatia sheria bila kushurutishwa.

“Sheria ya Mawasiliano iko wazi; ikiwa unahitaji kutoa huduma zozote za Mawasiliano katika nchi yetu sharti uwe na leseni, hivyo niwakumbushe wenzetu (watoa huduma) kuhakikisha wanakata leseni ndipo watoa hizi huduma,” alibainisha Afisa Mawasiliano.

Ushindani katika sekta ya posta kwa mara ya kwanza uliruhusiwa Tanzania mwaka 1989 kwa kutumia Sheria Posta na Simu ya wakati huo ambayo iliruhusu posta binafsi ya kwanza kusajiliwa na kuanza kutoa huduma. Mageuzi ya sekta ya mawasiliano yalianza rasmi 1994 ambayo iliweka ushindani wenye masharti yaliyowekwa na Mdhibiti wa Sekta. Kwenye miaka ya mwanzo ya 2000 makampuni binafsi mengi ya usafirishaji nyaraka, vipeto na vifurushi yalisajiliwa yakiwemo mabasi ya abiria. Hadi sasa kunawatoa huduma za Kiposta na Usafirishaji wa Vifurushi na Vipeto wapatao 96, likiwemo Shirika la Posta.

Post a Comment

0 Comments