Ticker

6/recent/ticker-posts

ZINGATIENI MASHARTI YA HATI MILKI ZA ARDHI-DKT MABULA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wananchi katika eneo la Shibula Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza wakati wa zoezi la kutoa hati tarehe 17 April 2023. Kulia ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Happy Mtutwa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati mmoja wa Milki ya Ardhi waliopatiwa hati katika eneo la Shibula halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza tarehe 17 April 2023. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala.
Baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Ilemela mkoa wa Mwanza waliojitokeza kupatiwa hati milki za ardhi wakati wa zoezi la utoaji hati lililofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika eneo la Shibula tarehe 17 April 2023.
Mkuu wa wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza Hassan Masala akizungumza katika zoezi la utoaji hati milki za ardhi lililofanyika eneo la Shibula manispaa ya Ilemela tarehe 17 April 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifurahia jambo na mwananchi ambaye ni shabiki wa timu ya Simba baada ya kumkabidhi hati katika eneo la Shibula manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza ikiwa ni siku moja baada ya Simba kuifunga Yanga bao 2-0.




Mmoja wa wananchi wa Ilemela akikabidhiwa hati na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa zoezi la kutoa hati kwa wananchi wa halmashauri ya Ilemela tarehe 17 April 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)






*******************

Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi wanaokabidhiwa hati milki za ardhi kuhakikisha wanazingatia masharti yaliyopo kwenye hati sambamba na kufuata mipango kabambe ya maeneo husika.

Dkt Mabula amesema hayo tarehe 17 April 2023 katika eneo la Shibula wilayani ilemela mkoani Mwanza wakati wa zoezi la kutoa Hati Milki za Ardhi kwa wananchi wa eneo hilo. Jumla ya Hati 570 ziliandaliwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa eneo hilo.

‘’Huwezi kupata hati leo, kesho unaenda kuomba kubadili matumzi mwisho wake miji inaonekana haina maana na haipendezi na sisi tunataka Jiji la Mwanza na Ilemela ikiwemo liwe mfano, tunapima viwanja vingi kwa ajili ya uwekezaji tuzingaite kilichopo kwenye Master Plan’’ alisema Dkt Mabula.

Amewaonya wanaopata hati milki za ardhi kutobadili matumizi na kuwaagiza watendaji wa sekta ya ardhi na uongozi wa wilaya ya Ilemela kuhakikisha hakuna kubadili matumizi na badala yake wamiliki wazingatie masharti ya hati na yale matumizi yaliyopo kwenye mpango kabambe.

Akigeukia suala la utoaji Hati Milki za Ardhi katika halmashauri ya Manispaa Ilemela, Dkt Mabula ameshangazwa na idadi ndogo ya wamiliki waliojitokeza kuchukua hati ambao ni 50 kati ya 570 walioandaliwa kuchukua hati.

‘’Watu wana tabia ya kulalamika hati hazitoki, tuna hati 570 hapa waliojitokeza ni 50 tu, hao wengine wako wapi ni kitu ambacho hakieleweki, hati zinaandaliwa lakini hamji kuchukua, hizo zinazobaki naomba muangalie namna mtakavyotoa.’ alisema Dkt Mabula

Ametaka wamiliki wa ardhi walioshindwa kuchukua hati kuandaliwa utaratibu maalum wa kupatiwa hati hizo huku akieleza kuwa, idara ya ardhi katika halmashauri ya Ilemela kwa kushirikiana na ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza kuchagua sehemu moja na kutumia wiki mbili kutoa hati kwa wahusika ili ziweze kuisha na kuendelea na hati nyingine ambazo ziko katika mchakato.

Aidha, waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameeleza kuwa wizara yake iko katika mageuzi makubwa ya kubadilisha mifumo yake lengo likiwa kuweka taarifa za ardhi sawa, kuondoa migogoro ya ardhi pamoja na kuwezesha serikali kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.

‘’Mifumo inaboreshwa na taarifa za sekta ya ardhi zinaenda kukaa vizuri na sasa taarifa ya kudaiwa kodi ya ardhi utaipata kupitia simu yako ya kiganjani na unapopata ujumbe nenda kalipe maana huhitaji kwenda ofisni’’ alisema Dkt Mabula

Kufuatia hatua hiyo, Dkt Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kutimiza majukumu yao na kusisitiza kuwa asingependa watanzania wenye shida kwenda ofisi za ardhi na kuelezwa njoo kesho na kuweka bayana kuwa kama suala haliwezekani ni bora kuelezwa ukweli.

Amesema. maboresho makubwa yamefanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wizara yake kupatiwa fedha nyingi hasa ikizingatiwa Wizara ya Ardhi ni wezeshi na isipowawezesha wananchi itamuangusha Mhe Rais na yeye asingependa kumuangusha.

Vile vile, Dkt Mabula amewataka wamiliki wa ardhi waliowekewa alama za mipaka (Beacons) katika maeneo yao kuhakikisha wanakamilisha taratibu za umilikishwaji ili waweze kupatiwa hati milki za maeneo yao kwa lengo la kuziweka ardhi zao salama.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni moja ya halmashauri nchini zilizonufaika na mkopo usio na riba kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ambapo katika awamu ya pili halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 3.589.


Post a Comment

0 Comments