Ticker

6/recent/ticker-posts

IFM, ACCA WASHIRIKIANA KUNOA WANAFUNZI KATIKA MASUALA YA UHASIBU NA FEDHA KWA VIWANGO VYA KIMATAIFA

NA MWANDISHI WETU

CHUO Cha Usimamizi wa Fedha nchini (IFM, ) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Uhasibu (ACCA,)wameendelea kutoa hamasa kwa wanafunzi wa Chuo hicho kupitia udhamini kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya Uhasibu na Fedha kwa ngazi zote pamoja na ACCA kukabidhi vitabu vya taaluma ya Uhasibu na Fedha maalum kwa wanafunzi wa ngazi zote za elimu zinazotolewa na chuo kwa lengo la kukuza taaluma hiyo Nchini, Barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Akizungumza na Michuzi Blog mara baada ya Warsha iliyowakutanisha na wanafunzi wanaosoma masomo ya Uhasibu na Fedha kuanzia ngazi ya Cheti hadi Shahada zinazotolewa na IFM jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa ACCA Tanzania Jenard Lazaro amesema; lengo la warsha hiyo ni kukabidhi vitabu vya taaluma ya Uhasibu na Fedha kwa uongozi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM,) ili wanafunzi waweze kunufaika na maarifa hayo kimataifa.

"Lakini pia, lengo la pili ilikuwa ni kuitambulisha taasisi ya ACCA ( The Association of Chartered Certified Accountants) kwa wanafunzi wa IFM ili waweze kunufaika na fursa hii kupitia Chuo hiki ambacho tumekuwa tukishirikiana kwa ukaribu." Amesema.

Amesema, wamekuwa wakishirikiana na IFM katika masuala mbalimbali yanayohusu taaluma ya Uhasibu na Fedha na kupitia warsha hiyo wanafunzi watapata fursa ya kupata mafunzo hayo na kuzidi kuimarisha sekta ya Uhasibu na Fedha nchini kwa viwango vya Kimataifa.

"ACCA inafanya kazi kwa ukaribu sana na uongozi wa vyuo hivyo ikiwemo IFM ili kuhakikisha inajenga uelewa katika taaluma ya Uhasibu na Fedha na hivyo kukuza na kuongeza idadi ya wataalam wa Uhasibu na Fedha hapa nchini Tanzania, Afrika na Duniani kwa ujumla." Amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uhasibu na Fedha wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM,)Dr. Erick Mwambuli amewataka wanafunzi kutumika fursa hiyo ya udhamini hususani katika punguzo la gharama za usajili na mitihani pamoja na kutumia vitabu vya masomo ya uhasibu na Fedha vilivyotolewa ili kujijenga kimaarifa zaidi kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Aidha amesema, kupitia mafunzo na udahili wa mitihani ya ACCA kutaongeza wigo wa wataalamu nchini na kuchangia katika kuboresha uandaaji wa taarifa za uhasibu.

“Ujuzi na maarifa yatakayopatikana yatakuwa ni nyenzo muhimu itakayoongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuendeleza taaluma ya uhasibu na kuongeza idadi ya wataalamu." Amesema.

Amefafanua kuwa, vitabu vya taaluma ya Uhasibu na Fedha vilivyotolewa na ACCA kwa chuo hicho vimesajiliwa na vinapatikana katika Maktaba ya chuo hicho vimebeba maarifa yatakayowasaidia wanafunzi kuanzia ngazi ya cheti (Certificate,) hadi Shahada (Degree,) zinazotolewa na chuo hicho na wanategemea kutoa wataalam wa masuala ya Uhasibu na Fedha katika soko la Kimataifa.

Ushirikiano huo baina ya ACCA na Chuo Cha IFM utaongeza idadi ya wataalamu wenye sifa ya uhasibu wa kimataifa na utaokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kuwasomesha wataalamu nje ya nchi na hiyo ni pamoja na kuwajengea wataalamu uwezo wa kushindana kimataifa lakini pia kwenda sambamba na viwango vya kimataifa ambavyo hubadilika mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.


Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Uhasibu Tanzania (ACCA,) Jenard Lazaro (kushoto) akikabidhi vitabu vya taaluma ya Uhasibu na Fedha kwa Mkuu wa idara ya Uhasibu na Fedha ya Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM,) Dr. Erick Mwambuli (kulia,) mara baada ya Warsha hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Uhasibu Tanzania (ACCA,) Jenard Lazaro akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM,) katika Warsha maalum ya kuitambulisha ACCA kwa wanafunzi hao pamoja na kukabidhi vitabu vya taaluma ya Uhasibu na Fedha kwa Chuo hicho. Ameeleza kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na IFM katika masuala mbalimbali ikiwemo kukuza taaluma ya Uhasibu na Fedha kwa viwango vya Kimataifa, Leo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa utafiti na ushauri wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM,) Dr. Shufaa Al-Beity akizungumza katika Warsha hiyo na kueleza kuwa ushirikiano huo utaongeza idadi ya wataalam wenye sifa ya Uhasibu wa Kimataifa, Leo jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments