Ticker

6/recent/ticker-posts

MCHENGERWA ATAKA KUANZISHWA IDARA YA KUPAMBANA NA UJANGILI, AZINDUA MIKAKATI YAKENa John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Mohamed Mchengerwa ametaka kuanzishwa kwa Kurugenzi maalum itakayoshughulikia masuala ya kupambana na ujangili wa wanyamapori ili kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na amemteua Kamshina Msaidizi wa Uhifadhi John Antony Nyamhanga kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kudhibiti Ujangili nchini.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Mei 31,2023 kwenye hafla ya uzinduzi wa mkakati wa kitaifa wa kudhibiti ujangili 2023- 2033 na mkakati wa usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyama za Jamii jijini Dodoma.

Amewaomba watanzania kuacha mara moja tabia ya ujangili na kusisitiza kuwa kwa sasa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kufanya ujangili.

Aidha, ameelekeza taasisi za uhifadhi chini ya Wizara yake (NCAA, TANAPA, TAWA na TFS) chini ya mfumo wa Jeshi la uhifadhi zishirikiane katika kutekeleza mikakati hiyo na kukamilisha mara moja Mkakati wa Kitaifa wa Rasilimali Fedha “Fund Raising Strategy” kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji Mikakati hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya kikao cha wadau wote wa uhifadhi ili kujadili kwa pamoja namna ya kutekeleza mikakati husika ili kila mdau aweze kufahamu majukumu yake.

Aidha, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye idadi kubwa ya wanyamapori na imetenga zaidi ya theluthi ya ardhi yake kwa ajili ya uhifadhi wa Wanyamapori hivyo ni muhimu kuwa na kurugenzi kamili ambayo itasaidia kulinda na kuhifadhi wanyamapori.


Amefafanua kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya simba, chui, nyati na ni ya tatu kwa idadi ya tembo duniani ambapo amesema hiyo inatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi wa wanyamapori.


Aidha, amesema utalii unachangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni na asilimia 17 ya pato la Taifa ambapo amesisitiza kuwa uhifadhi wa rasilimali hizi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla na amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuutangaza utalii kupitia Royal Tour.


Amesema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Mhe. Rais kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii hivyo kazi inayotakiwa kufanyika kwa sasa ni kuongeza vyumba vya kulala wageni na amewataka watanzania kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika eneo hilo.

Waziri Mchengerwa amesema Wizara kwa kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara imekuja na mikakati hiyo ili kuwezesha Serikali kudhibiti Ujangili na kushirikisha jamii katika uhifadhi.

Ameeleza kuwa mkakati wa kitaifa wa kudhibiti ujangili wa mwaka 2023 – 2033 unalenga kuudhibiti ujangili na biashara haramu ya nyara ndani ya nchi na kwenye maeneo ya mifumo ikolojia inayovuka mipaka ya nchi na kuimarisha uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori kwa kupunguza matukio ya ujangili kwa wanyamapori muhimu, kudhibiti uwindaji haramu wa nyamapori “vimolo” na kuhakikisha kuwa hakuna nyara inayokamatwa nje ya nchi ikitokea Tanzania.

Kwa upande wa Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMA) wa mwaka 2023 – 2033, amesisitiza kuwa unalenga kuhakikisha uhifadhi endelevu wa wanyamapori, ulinzi wa makazi yao ikiwa ni pamoja na kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori, kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, kuchochea maendeleo endelevu, kukuza utalii wa picha na uwindaji wa kitalii na kuboresha ustawi wa jamii zinazoishi karibu na maeneo ya WMA.
Amesema utekelezaji wa Mkakati huu unategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali fedha na watu pamoja na matumizi ya teknolojia. Hivyo, amewaomba wadau wa maendeleo, Asasi zisizo za Kiserikali na watu binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza Mikakati hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Kudumu ya Ardhi,Maliasili na Utalii Mhe. Mzava ameipongeza Wizara kwa kudhibiti ujangili na kuandaa mikakati hiyo ambapo pia amesisitiza ushirikishwaji wa jamii zinazozunguka hifadhi na kuzingatia ugawaji wa fedha za jumuiya za HIfadhi.


Aidha amesisitiza kuwa Kamati ipo tayari kushirikiana na Serikali wakati wowote inapohitaji msaada wake.Post a Comment

0 Comments