Ticker

6/recent/ticker-posts

VIJANA 24,458 WAPATIWA MAFUNZO YA JKT

Na Immaculate Makilika – MAELEZO


Serikali imesema kuwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeendelea kuwapatia vijana wa Kitanzania mafunzo ya ukakamavu, stadi za kazi, kuwajengea uzalendo na umoja wa kitaifa.

Ambapo, mafunzo yamefanyika kwenye kambi mbalimbali za JKT kupitia Operesheni Jenerali Venance Mabeyo. Jumla ya vijana 24,458 wa Mujibu wa Sheria wamepatiwa mafunzo, kati yao 17,942 wa kiume na 6,516 wa kike. Aidha, vijana 13 11,358 wa Kujitolea wamepatiwa mafunzo, kati yao 7,483 ni wa kiume na 3,875 ni wa kike.

Hayo yamesemwa leo Mei 24, 2023 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Jujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Aliongeza kuwa JKT imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kilimo (2019/2020 -2024/2025) ambao unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kujitosheleza kwa chakula ili kuipuguzia Serikali gharama za kulisha vijana wanaohudhuria mafunzo ya JKT na kuiwezesha nchi kuwa na akiba ya chakula.

“Kuwezesha Mkakati huo kutekelezwa ipasavyo JKT imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kupitia Mkataba wa Makubaliano katika maeneo ya teknolojia za kilimo, utafiti wa kilimo, uzalishaji wa mazao ya kimkakati na uzalishaji wa mbegu za chikichi, kahawa, mahindi, mpunga na alizeti. Utekelezaji wa Mkataba huo, umewezesha JKT kuongeza uzalishaji wa mazao husika”.Alieleza Mhe. Bashungwa.

Alifafanua kuwa JKT inashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuwawezesha vijana kupata ujuzi katika ufugaji wa nyuki ambapo Wakala wa Huduma za Misitu imeipatia JKT mizinga 100 ya kisasa ya kufugia nyuki.

Mhe. Bashungwa alitaja faida ya mafunzo hayo kwa vijana yanayotolewa na JKT kuwa yameimarisha umoja wa Kitaifa kwa kuwa Vijana wengi waliopitia JKT wameonesha moyo wa kupenda kazi za mikono, kujituma na kujiheshimu, kutoa wanamichezo bora, wenye viwango vya kitaifa na kimataifa na hivyo kuiletea nchi sifa.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yamesaidia kuwaandaa vijana kuwa tayari kuitumikia nchi katika majanga ikiwemo mafuriko, ajali za moto na ajali nyinginezo na kuwa mfano wa kuigwa na mataifa jirani na hivyo kuwa chachu kwa mataifa hayo kuanzisha shughuli za malezi ya vijana katika nchi zao ikiwemo Zambia na Msumbiji.

“Baada ya kumaliza muda wa mafunzo na kutumikia JKT, vijana waweze kurejea majumbani kwao wakiwa raia wema, wazalendo na wenye uwezo wa kujitegemea na kulilinda Taifa. Nitoe rai kwa vijana wote wanaopata fursa za kupata mafunzo haya, kuzitumia stadi za kazi na maisha walizozipata kujiajiri na kujitegemea”. Alisisitiza Mhe. Bashungwa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent L. Bashungwa (Mb) akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024. Leo tarehe 24 Mei 2023.

Post a Comment

0 Comments