Ticker

6/recent/ticker-posts

WADAU WA NYUKI NCHINI WAHIMIZWA KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA NYUKI DUNIANI MKOANI SINGIDA

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras akizungumza wakati wa Kikao cha Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani kilichofanyika leo mkoani Singida
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi wa Mkoa wa Singida, Stanslaus Choaji akizungumza namna ambavyo mkoa wa Singida umejipanga kuadhimisha siku ya Nyuki Duniani kwenye Kikao cha kamati ya maadhimisho hayo kilichofanyika leo mkoani Singida.

Wajumbe wa Kamati ya Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani wakijadili masuala mbalimbali ya namna ya kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, leo mkoani Singida

Na Mwandishi Wetu, Singida.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa wito kwa Wananchi wote kushiriki maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani huku ikisisitiza kuwa Maadhimisho hayo yatakuwa na faida na matokeo chanya kwa Wadau wa Sekta ya Misitu na Ufugaji nyuki nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras mara baada ya kufanyika kwa kikao cha pamoja cha kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo ambapo amesema maadhimisho ya mwaka huu yatakuwa ya namna yake.


Maadhimisho hayo yatatanguliwa na maonesho ya huduma na bidhaa mbalimbali za mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki kuanzia Mei 18 hadi Mei 21 ambapo wananchi watapatiwa mafunzo ya ufugaji nyuki na kuelezwa faida za mazao ya mdudu nyuki.

“Tunashirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani. Kilele chake huwa ni Mei 20 ya kila mwaka, lakini kama nchi maadhimisho haya yataanza Mei 18 hadi Mei 21, 2023 hivyo wananchi wa Singida na mikoa jirani karibuni sana” amesema.

Akizungumzia siku hizo nne za Maadhimisho, Mkurugenzi Pancras amesema kutakuwa mada mbalimbali zitakazojadiliwa ikiwemo kuangalia namna bora ya kutunza na kuchakata mazao ya nyuki huku akisisitiza kuwa wadau mbalimbali wameshathibitisha ushiriki wao kwa ajili ya kushiriki zoezi hilo muhimu kwa wafugaji nyuki wote hapa nchini.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi wa Mkoa wa Singida, Stanslaus Choaji amesema maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea kupamba moto huku akiwataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi.

“Wananchi wa Singida mjipange kutumia fursa hii ya maadhimisho haya kiuchumi ili mkoa uwe kinara kwa ufugaji nyuki nchini.” amesisitiza

Post a Comment

0 Comments