Ticker

6/recent/ticker-posts

BODI ZA VYAMA VYA USHIRIKA WA MAZAO YA BUSTANI WAPEWA SHULE

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Arusha Grace Masambaji akifungua mafunzo ya Ushirika kwa Wajumbe wa Bodi za Vyama vya Ushirika wa mazao ya Bustani, Mkoani Arusha.

Afisa Ushirika Ndimolwo Laizer akielezea misingi ya Ushirika Kimataifa kwa Wajumbe wa Bodi wa Vyama vya Ushirika wa mazao ya Bustani Mkoani Arusha.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Kanti Kimario akitoa mada kuhusu masuala ya Wajibu wa Wajumbe wa Bodi, Mkoani Arusha.

Na.Mwandishi WetuMrajis Msaidizi wa Mkoa wa Arusha Grace Masambaji amewataka Wajumbe wa Bodi za Vyama vya Ushirika wa mazao ya Bustani kuvisimamia Vyama vya Ushirika vya Ushirika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za Ushirika ili kuhakikisha Vyama hivyo vinaimarika na kukuza Uchumi wa Wanaushirika.

Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Wajumbe wapya Bodi wa Vyama vya Ushirika vya mazao ya Bustani wa Mkoa wa Arusha Juni 5, 2023 ametoa wito kwa Viongozi hao wa Vyama vilivyosajiliwa karibuni kutumia fursa ya mafunzo ya Ushirika yanayoendeshwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kupata maarifa ya kusimamia vizuri vyama hivyo ili viweze kujiendesha kwa tija.

Amewataka viongozi hao kujua mambo ya msingi kuhusu Sheria ya Ushirika, masharti ya vyama, taratibu za uandaaji wa Vitabu vya vyama, kaguzi za vyama ili vyama viweze kujiendesha kwa usahihi na hatimaye viwe sehemu ya Vyama vinavyopata hati safi inayotafsiri utendaji mzuri wa Chama.

Nae Afisa Ushirika Laizer Ndimolwo katika mafunzo hayo ameeleza umuhimu wa Ushirika akifafanua kuwa ni nyenzo ya kuwaunganisha watu kwa pamoja ili kutatua changamoto fulani na hatimaye kujikomboa kiuchumi.

Aidha, ameeleza kuhusu misingi ya Ushirika Kimataifa akizungumzia Ushirika ni hiari na wenye uanachama wa wazi, Ushirika kufuata makubaliano ya kidemokrasia, ushiriki wa shughuli ya kiuchumi, elimu na mafunzo, Ushirikiano baina ya Vyama pamoja na kujali jamii.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi Kanti Kimario akitoa mada mada wakati wa mafunzo hayo ameeleza sifa za Wajumbe wa Bodi za Vyama vya Ushirika kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za ushirika akianisha baadhi ya sifa hizo ni pamoja na wajumbe wa Bodi kuzingatia kutokuwa na mgongano wa kimaslahi unaoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya ushirika, kulipa hisa zinazohitajika kwa mujibu wa masharti ya Chama, ushiriki wa wajumbe katika vikao vilivyowekwa kwa mujibu wa masharti.

Sambamba na mada hiyo ameeleza Wajibu wa Wajumbe wa Bodi ikiwa ni pamoja na utunzaji sahihi wa taarifa, nyaraka, usimamizi wa kulipa kodi, uandaaji wa mikutano mikuu ya Chama, kuwezesha ukaguzi wa Vitabu vya Hesabu kwa aliyeidhinishwa kufanya hivyo, kuandaa mpango mkakati wa wa Chama na Mpango kazi wa kila mwaka.akisisitiza Wajumbe kuwakilisha maslahi na mahitaji ya wanachama wa Chama cha Ushirika.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Mang’ola Endaghan Athumani Salum amepongeza mafunzo hayo kwani wamepata fursa ya kujifunza na kuelewa dhana nyingi za Ushirika. Ameongeza kuwa Wanaushirika wana Imani kubwa kuwa Ushirika huo unaenda kuwasaidia katika kutatua changamoto yao kubwa ya upatikanaji wa masoko ya mazao yao ya bustani pampja na upatikanaji wa pembejeo.

Wajumbe wa Bodi takribani 97 kutoka Halmashauri za Wilaya Meru, Arusha, Karatu wanaendelea kupata mafunzo hayo yanayoendelea Jijini Arusha hadi Juni 7, 2023. Mkoani Arusha tayari Vyama vya mazao ya bustani zaidi ya 15 vimesajiliwa huku zoezi la usajili huo likiendelea kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika Na.6 ya 2013. Mazao ya Bustani ni pamoja na mbogamboga, maua, matunda

Post a Comment

0 Comments