Ticker

6/recent/ticker-posts

GAZETI LA MWANAHALISI KUINGIA MTAANI JUNI 29,2023

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya HaliHalisi Publishers linalochapisha gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kulifungulia gazeti hilo pamoja na magazeti mengine ambayo yalikuwa yanefungwa na Serikali ya mtangulizi wake.

Akizungumza leo Juni 28,2023 Jijini Dar es Salaam, ameiomba Serikali na Mamlaka zake endapo litaona gazeti hilo limeandika habari zenye mapungufu au zinazohitaji ufafanuzi wake, kutoa ushirikiano kwa kuandika taarifa za ufafanuzi kisha gazeti lake litaziandika ili kuweka uwiano sawa.

"Sisi tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uvumilivu wake na kukubali gazeti kama MwanaHalisi kurudi mtaani, sababu sisi tokea awamu ya Rais Jakaya Kikwete tumekuwa tukisimama kwa ajili ya Umma na kuandika habari za kweli, sahihi na zinazopendwa na watu wengi". Amesema Kubenea.

Aidha Kubenea amesema gazeti hilo linatarajiwa kuanza kurejea mtaani Juni 29, 2023 baada ya kuwa kifungoni kwa takribani miaka sita tangu lilipofungiwa na Serikali Septemba 2017.

Amesema Gazeti la MwanaHalisi litakuwa linatoka mara moja kila wiki kwa siku ya Alhamisi.

Pamoja na hayo Kubenea amezipongeza taasisi ikiwemo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari la Tanzania (MCT), viongozi wa dini na wananchi waliopaza sauti zao kuiomba Serikali iyatoe kifungoni magazeti yaliyofungiwa.


Post a Comment

0 Comments