Na Okuly Julius-Dodoma.
KAMATI ya utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania CWT)Taifa,imeazimia kwa pamoja kuweka zuio kwa Katibu Mkuu wa Chama hicho Japhet Maganga kuendesha shughuli zozote za Chama hicho hasa katika masuala ya fedha na utawala.
Maazimio hayo yamefanywa na Wajumbe wa Kamati 18 toka mikoa 18 nchini ambapo wametoa maazimio hayo leo June 6,2023 Jijini hapa.
Hatua hiyo ni kufuatia kuwepo kwa madai ya uongozi wa Juu kuvunja Katiba ya CWT hivyo Kamati hiyo kuelekeza shughuli zote za CWT kufanywa na Naibu Katibu Mkuu Joseph Msalaba.
Wakiongea mbele ya Waandishi wa Habari mara baada ya kukutana katika ofisi za chama hicho,wamesema wamejiridhisha kuwa uongozi uliopo madarakani unavunja Katiba na kanuni zake.
Akizungumza kwa niaba ya wengine Mwenyekiti wa muda wa kikao hicho ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo na mwakilishi wa walimu wa Mkoa wa Njombe Mwl.Tobias Sanga amesema kikao hicho kimeridhia kumzuia Katibu Mkuu wa CWT kutoendesha shughuli za Chama hicho Kutokana na uonevu anaoufanya kwa wanachama wake.
Amefafanua kuwa moja ya ajenda ya kikao hicho ni uhamisho holela wa wafanyakazi, kuhusu matumizi holela ya michango ya walimu pamoja kutaka mkutano Mkuu wa dharula bila mafanikio .
"Tumejiridhisha na tumeona utendaji kazi wa Katibu huyu hauko sawa,tumepitia miongozo yetu tumejiridhisha,tunachukizwa kuona fedha za 2% za walimu zinatumika bila utaratibu,tukihoji hatupewi Ushirikiano,"amesema Mwalimu huyo.
Pamoja na mambo mengine Sanga amesema,"Kwa Mamlaka tuliyonayo tumekubaliana kazi zetu zitafanywa na Naibu Katibu mkuu ambaye atasimamia masuala yote ya utawala na fedha,"amesisitiza.
Amefafanua kuwa,"Naomba nieleweke wazi kuwa hatuna shida na Katibu Mkuu ila tunachotaka ni mfumo wa utendaji,tunataka walimu tunao wawakilisha wapate haki zao na sio unyanyasaji unaoendelea,"amesema
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CWT-Taifa Joseph Msalaba ambaye ndiye amepewa Mamlaka ya utendaji amesema kuwa amelipokea suala hilo na kueleza kuwa kikao hicho kimefanyika kwa amani kama ilivyotarajiwa.
Amesema "nimepokea uwepo wa ujio wa Wajumbe hawa 18 wa Kamati ya utendaji Taifa japo walitakiwa kuwa 38 lakini hakuna kilicho haribika,"amesema
Naye Mwalimu Sabina Lipukila ambaye ni mwakilishi wa walimu wa Ruvuma amesema mgogoro uliopo unasababisha utendaji kazi wa walimu kushuka na kusisitiza kuwa kwa ujumla Katiba yao haiendi wanavyotaka.
Amesema uhamisho wa Makatibu unafanywa kiholela bila wao kushirikishwa na kueleza kuwa jambo hilo linashusha ari ya kufanya kazi kwa weledi Kutokana na hofu ya uhamisho.
"Hakuna asiyefahamu kuwa sisi ni chombo cha ajira,kuna vitu vingi tunavifuatilia haviendi sawa,kwa muda mrefu sasa tumekuwa tunaomba kikao lakini tumenyimwa,tungekubaliwa vikao haya yote tungezungumza na kuyamaliza kule,"amefafanua
Kwa upande wa Mwanasheria wa Chama hicho Paschal Msafiri amesema kuwa wenye Mamlaka ya kuitisha vikoa vya dharura ni Rais au Katibu Mkuu tena pale wanapoona kwamba kuna dharura kweli sasa ukisikiliza yote wanayolalamikia hayana udharura wa kuitisha kikao hicho.
"Kikao kilichofanyika ni batili kwani hakiko kwenye mfumo Mimi ningewashauri kuhifadhi hizo agenda zao ili ifikapo Julai ambapo ndio Mwezi wa kufanya kikao Cha pili kama katiba ya chama inavyoelekeza kifanye vikao viwili Kwa Mwaka na tayari Cha kwanza kilifanyika Mwezi Januari na Cha pili kitafanyika Mwezi wa Julai hivyo pale ndipo wangeweza kuomba kuingizwa Kwa agenda hiyo ila Kwa sasa ni naweza kusema kikao hicho ni batili,"
Na kuongeza kuwa" Kamati Tendaji Taifa sio mamlaka halali ya kumjadili Katibu Mkuu, wao wanachotakiwa kufanya ni kuandaa ajenda hiyo na kuipeleka kwenye Baraza la Taifa ndio wanaoweza kujadili na kama wataona yeye au kiongozi yeyote ana matatizo basi wao kama Baraza Katiba imewapa mamlaka ya kumsimamisha au kumuwajibisha kulingana na makosa yake lakini hiki kilichofanyika leo ni kinyume na Katiba”alieleza Mwanasheria huyo.
Pia ametoa wito Kwa walimu wote na wanachama wa Chama hicho kuwa watulivu na kuendelea kufanya kazi huku wakisubiria Mkutano Mkuu wa Chama utakaofanyika Mwezi Julai.
0 Comments