
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na Wafanyakazi wa Benki ya NMB kabla ya kupokea Gawio la Serikali Shilingi Bilioni 45.5 kutoka Benki hiyo katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mafanikio ya Benki Mlimani City Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Juni, 2023.




Viongozi mbalimbali pamoja na Wafanyakazi wa NMB wakiwa kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Mafanikio ya Benki hiyo Mlimani City Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Juni, 2023.
********************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika yote ya umma kujiendesha kwa ufanisi, tija na ushindani ili yaweze kuwa endelevu.
Rais Samia ametoa tamko hilo leo wakati wa hafla ya benki ya NMB ya kukabidhi gawio kwa Serikali na kusherehekea miaka 25 ya safari ya mafanikio ya benki hiyo, iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini ya utendaji wa mashirika yote ya umma na yale ambayo Serikali ina hisa kubwa ili kubaini mashirika yasiyo na faida yanayoshindwa kujiendesha na kuitia hasara Serikali.
Rais Samia pia amesema tathmini hiyo inafanywa na Msajili wa Hazina ambapo Serikali itayachukulia hatua na kuyafuta mashirika ambayo hayafanyi vizuri, kuyasaidia na kuyapa miongozo ya namna ya kujiendesha ili yapate faida.
Rais Samia amewataka wajasiriamali, wakulima na wananchi wote wanaohudumiwa na benki ya NMB kuendelea kuwa waaminifu wanapochukua mikopo bila dhamana ili benki hiyo iendelee kuwa na ustawi.
Benki ya NMB imekabidhi gawio la shilingi bilioni 45.5 ambapo Serikali inamiliki 31.8% ya hisa katika benki hiyo huku asilimia zingine zikiwa zinamilikiwa na wadau kutoka sekta binafsi.
0 Comments