Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUFANYIA KAZI CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA UFUGAJI NYUKI

Afisa Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na utalii wa Dawati la Sera pamoja na Sheria, Filipo Mwampamba ,akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa wadau wa nyuki wa siku mbili uliozikutanisha sekta za Umma na Binafsi leo Juni 7, 2023 Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali linashugjulikia maendeleo ya Sekta ya Ufugaji Nyuki, Linus Gedi, akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa nyuki wa siku mbili uliozikutanisha sekta za Umma na Binafsi leo Juni 7, 2023 Jijini Dodoma.

Mwakilishi kutoka Bevac akifuatilia mkutano wa wadau wa nyuki wa siku mbili uliozikutanisha sekta za Umma na Binafsi leo Juni 7, 2023 Jijini Dodoma.


Washiriki mbalimbali wakifatilia mkutano wa wadau wa nyuki wa siku mbili uliozikutanisha sekta za Umma na Binafsi leo Juni 7,2023 jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zinazoikabili sekta ya ufugaji nyuki lengo likiwa ni kuongeza hamasa ya wadau wengi kuingia katika sekta hiyo ili kufungua fursa ya ajira kwa vijana pamoja na kusaidia kuleta fedha za kigeni.

Hayo yamesemwa na Afisa Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na utalii wa Dawati la Sera pamoja na Sheria, Filipo Mwampamba wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Juni 7, 2023 Jijini Dodoma mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa wadau wa nyuki wa siku mbili uliozikutanisha sekta za Umma na Binafsi.

Amesema miongoni mwa mambo ambayo wadau wameiomba Serikali ifanyie kazi ni pamoja na changamoto ya uwepo wa tozo nyingi wakati wa kupeleka mazao ya nyuki nje ya nchi , pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kuchakatia mazao hayo.

“ Katika mkutano huu Wadau wamebainisha changamoto ya uwepo wa maeneo yanayofaa kwa ajili ya kuchakatia mazao pamoja na upatikanaji wa vifungashio ambavyo ukiangalia changamoto hizo tayari tumeanza kuzifanyia kazi.” amesema.

Ameongeza kuwa Mkutano huo umetoa fursa kwa Wadau hao kuwasilisha changamoto zao wanazokumbana nazo pamoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kushughulikia changamoto hizo ikiwa mkutano wa kimkakati chini ya ufadhili wa Mradi wa Umoja wa Ulaya ujulikanao kwa jina la BEVAC

“ Sisi kama Serikali tupo hapa kwa lengo la kusikiliza lakini pia kupokea ushauri na kisha kufanyia kazi kwa karibu ili kuchagiza uwekezaji katika ufugaji nyuki, Tunaishukuru Serikali ya Umoja wa Ulaya kwa kuwezesha vikao hivi muhimu.” ameongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali linashugjulikia maendeleo ya Sekta ya Ufugaji Nyuki, Linus Gedi, amesema kupitia mkutano huo umekuwa muhimu sana kwao kwa vile wamepata fursa kuzungumzia vikwazo wanavyopitia wauzaji wa bidhaa za nyuki ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

“ Kuna taratibu ndefu sana ambazo wauzaji wa mazao ya nyuki wanapitia mpaka mzigo wake uingie kwenye meli na kwenda kwenye masoko, Tunataka Serikali itupunguzie huu mchakato ili biashara hii iwe na tija.” amesema.

Pia, amesema wameangalia vikwazo ambavyo vipo katika uchakataji wa mazao ya nyuki ambavyo vinafanya bidhaa zisiwe bora na shindani katika masoko ya ndani na nje.

“ Ni matarajio yetu kwamba kero zinazowasumbua zitapata ufumbuzi na wafanyabiashara watafurahia na kupata faida katika biashara yao .” amesisitiza Mwenyekiti Gedi

Post a Comment

0 Comments