Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Suzan Mkangwa akizungumza na Uongozi wa Kiwanda hicho.
Kamishina wa Kazi Ofisi ya Waziri Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Suzan Mkangwa akiangalia bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda hicho
Kamishina wa Kazi Ofisi ya Waziri Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Suzan Mkangwa akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kazi Wafawidhi, Menejimenti ya Kiwanda cha A to Z Textile Mills walipotembelea Kiwanda hicho, kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho.
Na: Mwandishi wetu - Arusha.
Kamishina wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Suzan Mkangwa ameutaka uongozi wa kiwanda cha A to Z Textile Miles Limited kutoa mikataba ya Ajira kwa wafanyakazi 131 wa kiwanda hicho kama ambavyo sheria za kazi zinavyoelekeza.
Agizo hilo limetolewa Juni 28, 2023 Jijini Arusha alipotembelea kiwanda hicho, akiambatana na Maafisa Wafawidhi kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kubaini baadhi ya wafanyakazi hao hawajapewa mikataba ya Ajira.
Aidha, Mkangwa ameusihi uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha wafanyakazi wa kigeni katika kiwanda hicho wanatekeleza takwa la kurithisha ujuzi kwa wafanyakazi wazawa.
Sambamba na hayo, ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha unaboresha sera za uendeshaji wa kiwanda hicho kwa kushirikisha wafanyakazi, viongozi wa Chama vya Wafanyakazi wa kiwanda na TUICO ili sera hizo ziendane na sheria za kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu kutoka kiwanda hicho Mzee Justus ameahidi kuyafanyia kazi maagizo hayo kabla ya mwezi septemba, 2023.
0 Comments