Ticker

6/recent/ticker-posts

WANAWAKE WATUMIKA KATIKA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA YABAINIKA , DCEA YATOA ONYO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kutokana na udhibiti kuwa mkubwa wanaoendelea kuufanya katika biashara ya dawa za kulevya, wafanyabiashara wa dawa hizo wameendelea kubuni mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya ili kukwepa kukamatwa ikiwemo ya raia wa kigeni kuwatumia wanawake wa kitanzania kufanya biashara hiyo.

Akizungumza leo Juni 19,2023 mbele ya waandishi wa habari Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema baada ya kubaini mbinu hizo wamechukua hatua za kuzidhibiti huku akitoa onyo kwa wanawake ambao wanatumiwa na raia wa kigeni kufanyabiashara ya dawa za kulevya.

“Mbinu mojawapo inayotumika ni raia wa kigeni kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na wanawake wa kitanzania zaidi ya mmoja na kuficha dawa za kulevya kwenye makazi ya wanawake hao huku wao wakipanga nyumba tofauti na wanakoishi wapenzi wao.

“Hali hii husababisha wanawake wa kitanzania kuingia kwenye matatizo makubwa ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria huku wanaume wakiwakana wanawake hao. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imejipanga kikamilifu kupambana na biashara ya dawa za kulevya,”amesema Kamishina Jenerali Lyimo.

Aidha amesema wote wanaojihusisha au wenye mpango wa kujihusisha na biashara hiyo, waache mara moja au wajisalimishe wenyewe kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria.Pia, wananchi wanapaswa kuwa makini na mizigo wanayopewa kubeba au kuhifadhi pasipo kujua ndani yake kuna nini.

“Wanawake wanatakiwa kuwa makini zaidi kwani katika baadhi ya matukio, wamekuwa wakitumiwa na wapenzi wao hasa raia wa kigeni kusafirisha na kupokea mizigo wasiyoijua na wakati mwingine mizigo hiyo huwa na dawa za kulevya na hivyo hujikuta matatani.

“Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinaeleza kwamba, ni kosa kusafirisha dawa za kulevya, na mtu yoyote akithibitika kutenda kosa hilo atawajibishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 30 au kifungo cha maisha gerezani,”amesema.

Aidha amesema Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha inamaliza tatizo la dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii.Kutokana na kuwepo madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Ameongeza ni vema wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwafichua wote wanaojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya ili kwa pamoja tuweze kulikomboa taifa kutoka katika janga hilo na

katika kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya yanatokomea nchini, Mamlaka imejikita katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa jamii.

Amesema lengo ni kupanua wigo wa utoaji elimu huku akifafanua Mamlaka imeingia makubaliano na TAKUKURU kutumia klabu zao zilizokwisha anzishwa kwenye shule na vyuo kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya. Hivyo, elimu ya kupambana na rushwa na dawa za kulevya itatolewa kupitia klabu hizo.

Post a Comment

0 Comments