Ticker

6/recent/ticker-posts

BILIONI 37 KUMALIZA KERO ZA BARABARA TANGA, MENEJA TARURA AMSHUKURU RAIS.



Na Hamida Kamchalla, TANGA. 

BAJETI ya sh bilioni 37 iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2023/24 kupitia Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) Mkoa wa Tanga itaweza kusaidia kumaliza miradi ya kimkakati ya kuondoa vikwazo katika halmashauri saba mkoani humo.

Akiongea ofisini kwake Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga George Tarimo amesema bajeti iliyoidhinishwa ni mara tatu zaidi ya ile ya mwaka uliopita ambapo itakwenda kuboresha na kufungua miundombinu mingi zaidi katika ujenzi.

"Kwa upande wa miradi mingine ya kimkakati tuna mradi wa kuondoa vikwazo ambapo kuna halmashauri saba za Wilaya ambazo ziko katika hatua ya mwisho kuzitangaza, hizi kazi zinaratibiwa na kitengo maalumu ambacho kiko maka makuu Dodoma" amesema.

"Tunashukuru sana serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Tanga bajeti yetu imeongezeka mara tatu zaidi na imeweza kufungua barabara nyingi, huku ikiboresha barabara zilizokuwa vumbi kwenda kiwango cha changarawe na changarawe kwenda lami" amebainisha Tarimo.


Aidha Tarimo amefafanua kwamba mbali ya kufungua barabara pia kuna ujenzi mkubwa wa daraja la Mkomazi lenye urefu wa takribani mita 40 ambalo limegarimu kiasi cha zaidi ya sh bilioni 3.8 na sasa liko katika hatua ya kumwaga zege na tayari weka chuma.


Amesema serikali imedhamiria kuboresha mfumo wake wa manunuzi (Nest) katika utangazaji wa zabuni kwa mwaka huu wa fedha ambao umeanza Julia 1 na kwa Mkoa wa Tanga sasa wako mbioni kuanza kutangaza zabuni kwa Makandarasi kupitia mfumo huo ambapo baadhi yao wameshaanza kuleta maombi.


"Mpango tulionaoendelea nao sasa hivi ni kukamilisha maandalizi ya zabuni ili tuweze kutangaza, serikali imeboresha mfumo wa utangazaji wa zabuni kutoka katika mfumo wa zamani wa manunuzi (TaNePS) na sasa tunatangaza kupitia mfumo mpya wa (Nest), na tayari tumeshaanza" amesema.


Tarimo amesema utekelezaji wa mwaka wa fedha 2022/23 ulikwenda vizuri mbali na kero ndogondogo zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo hasa katikati ya jiji la Tanga ambako kulikuwa na maeneo korofi hasa katika kipindi cha mvua kubwa.


"Tunashukuru hali ya barabara zetu nyingi ziko shwari kwa sasa, utekelezaji umeenda vizuri maeneo yaliyobaki makorofi ni machache lakini kupitia bajeti yetu tumeweza kufungua njia nyingi ambazo zilikuwa na vikwazo na sasa hali siyo mbaya kwamba zinapitika muda wote" amesema.


"Maeneo mengi yaliyokuwa yanalalamikiwa kwasasa yapo vizuri, hivyo nina imani utekelezaji wa mwaka huu wa fedha utakwenda kuleta chachu katika ufanisi wa shuhuli zetu kwani kwa kiasi kikubwa tunaangalia miradi ya kimkakati ambayo nayo imeshaanza kutekelezeka" amesisitiza

Post a Comment

0 Comments