Ticker

6/recent/ticker-posts

BRELA YAIBUKA KIDEDEA MAONESHO YA 47 YA BIASHARA YA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Uwezeshaji wa Ukuzaji wa Biashara na Uwekezaji na kuibuka mshindi wa nne katika kipengele cha Banda Bora katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam yaliyofanyika katika uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Tuzo za ushindi huo zimetolewa tarehe 13 Julai 2023 na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, wakati wa kufunga maonesho hayo.

Katika kipengele cha Uwezeshaji wa Ukuzaji wa Biashara na Uwekezaji waliochukua nafasi ya pili ni Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) wakifuatiwa na Mamlaka ya Rufaa ya Manunuzi ya Umma (PPAA),wakati kwa upande wa Mabanda bora waliochua nafasi ya kwanza ni banda la Algeria, ikifuatiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) nafasi ya tatu ilichukuliwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).

Ushindi wa nafasi ya kwanza kwa BRELA ni mwendelezo wa jitihada za Taasisi katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na wadau wake, ambapo katika Maonesho ya 46 BRELA ilipata ushindi wa nafasi ya pili katika kipengele hicho hicho cha Uwezeshaji wa ukuzaji wa Biashara na Uwekezaji.

Kabla ya kufunga Maonesho hayo, Rais Mwinyi alitembelea Banda la BRELA ambapo alipata fursa ya kuona jinsi Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS) unavyofanya kazi. Pia alitumia nafasi hiyo kukabidhi Cheti cha Usajili kwa mmoja wa wafanyabiashara waliofika katika Banda la BRELA na kupata huduma ya usajili wa papo kwa papo zilizotolewa wakati wa Maonesho hayo kiwanjani hapo.

Post a Comment

0 Comments