Na Ashrack Miraji, Same
SERIKALI imetumia helkopta kutafuta makundi ya tembo waharibufu waliozagaa katika vijiji 25 vya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na kuwavisha vifaa maalum vya mawasiliano kufuatilia mwenendo wao.
Zoezi hilo la utafutaji tembo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengera alilotoa hivi karibuni alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika wilaya hiyo, ambapo aliagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kupeleka helkopta kusaidia zoezi.
Akizungumzia oparesheni hiyo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emmanuel Moirana amesema kwa siku ya kwanza jumla ya makundi matano ya tembo yamerejeshwa hifadhini na mkakati uliopo ni kuendelea na zoezi hilo kuondoa changamoto ya mara kwa mara kuripotiwa makundi hayo kuonekana maeneo ya nje ya hifadhi.
Amesema oparesheni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano baina ya taasisi nne zilizo chini ya wizara ya maliasili na utalii, kamati ya ulinzi na usalama wilaya na wananchi wenyeji ambao wanasaidia kuainisha maeneo walipo tembo.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amepongeza jitihada za wizara kwa uharaka wa kutekeleza ahadi ya kuondoa tembo hao kwa kuongeza vitendea kazi na rasilimali watu, akisema huenda changamato ikapungua na wananchi kuweza kuendeea na shughuli za uzalishaji.
Taarifa iliyowasilishwa na mkuu wa wilaya ya Same kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mchengerwa alipofanya ziara Julai 5, 2023 zinaeleza kuongezeka kwa matukio ya tembo kuvamia kwenye maeneo ya makazi.
Mkuu wa wilaya huyo amesema hadi sasa ekari 1m121.9 zimeharibiwa ambapo mwaka 2014 ekari 17 za mazao ziliharibiwa, 2015 ekari 22.5, 2016 ekari 27, 2017 ekari 125, 2018 ekari 421.5, 2019 ekari 757.25 na kifo cha mtu mmoja, 2020 ekari 421.5, 2021 ekari 475.25 na vifo vya watu wawili, 2022 ekari 620.9 na vifo vya watu wawili, wengine wawili kujeruhiwa sambamba na vifo kwa mifugo mitano na mwaka 2023.
Baadhi ya wazazi wa Wilaya ya Same walioshiriki katika oparesheni hiyo wamesema kuna idadi kubwa ya tembo ambao wametoka kwenye maeneo ya hifadhi na kufanya makazi ya kudumu kwenye maeneo ya vijiji, hali ambayo imesababisha baadhi yao hasa wakulima mwaka huu kukosa mazao.
“Madhara ya watu kuuliwa na tembo hapa kitongoji cha Kabambuu ni makubwa lakini hata kuvuna hatutavuna kwani wamekula mazao,” alisema Sallum Omary Mwenyekiti wa kitongoji hicho.
0 Comments