Ticker

6/recent/ticker-posts

TIC KUDUMISHA MAHUSIANO YA UWEKEZAJI NA INDIA

Na Beatrice Sanga - MAELEZO

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesaini Mkataba wa Makubaliano (Momerundum of Understanding (MoU)) na nchi ya India kupitia Idara ya Ushirikiano wa Nje na Serikali ya jimbo la Haryana (FCD, GOH) ikiwa ni kuelekea katika kusaini mikataba mbalimbali ya uwekezaji na kuvutia wawekezaji kutoka India kuja kuwekeza nchini.

Hayo yameelezwa na Gilead Teri Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) katika Makao Makuu ya Kituo hicho Jijini Dar es Salaam, alipokutana na wawekezaji kutoka jimbo la Haryana ambapo mbali na kusaini mkataba huo, wamefika nchini kuhudhuria maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Maarufu Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na historia ya maonesho ya sabasaba, wawekezaji zaidi ya sitini kutoka India wamekuja nchini kwaajili ya kutafuta fursa za uwekezaji, baadhi yao wameshiriki maonesho ya sabasaba lakini kwa kushirikiana na ubalozi wetu ulioko India pamoja na serikali ya Jimbo la Haryana, tumefanikiwa kuwashawishi wawekezaji zaidi kuja kuangalia fursa za uwekezaji, malengo yakiwa ni kuongeza ushirikiano kati ya taasisi zetu na taasisi ambazo ziko kwenye jimbo lao ili kukuza uwekezaji na kuleta uwekezaji hapa nchini,” ameeleza Teri

Teri amesema kuwa MoU iliyosainiwa itatumika kama Mfumo Mkuu wa kisheria wa kudhibiti uhusiano wa Tanzania na India kwa kuzingatia maeneo yaliyokubaliwa ya uwekezaji na kwamba wamejipanga kuongeza ushirikiano kati ya tanzania na serikali ya jimbo la Haryana.

“Maeneo ya uwekezaji yaliyokubaliwa chini ya Makubaliano haya ni pamoja na; Magari, Madawa, Viwanda vya Nguo, Vifaa vya Uhandisi/Mashine, nishati, kemikali na mbolea, uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, sayansi, elimu, utalii na maeneo mengine yenye maslahi kwa pande zote, ni matarajio yetu kuwa kusainiwa kwa Makubaliano haya kutafungua zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na India katika masuala yanayohusiana na uwekezaji, tumekubaliana kwamba, kabla ya mwezi wa tisa kutakuwa na uwekezaji ambao tayari utakuwa umekuja nchini na kuanza kufanya kazi.” Amefafanua Teri.

Aidha, Teri amesema kuwa wataishawishi serikali ya jimbo la Haryana kuja kuwekeza katika kongani za viwanda, kutokana na kwamba jimbo hilo ndilo lenye Kongani za viwanda nyingi zaidi nchini India kuliko jimbo lolote.

Kwa upande wake Dkt. Raja Sekhar Vundru Mkuu wa Msafara Serikali ya Jimbo la Haryana na Katibu Kiongozi wa Idara ya Mambo ya Ushirikiano wa Nje amesema kuwa kutokana na Tanzania kuzidi kupiga hatua katika masuala ya uwekezaji na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kumewasukuma serikali ya jimbo hilo kuja kuwekeza nchini.

“Uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi yetu ndiyo sababu kuu imechangia sisi kuja kutafuta fursa za uwekezaji hapa Tanzania, tuko hapa kama serikali ya jimbo la Haryana kutoka India, ambalo ni miongoni mwa majimbo yaliyoendelea zaidi kiviwanda nchini India, naamini huu ni mwanzo mzuri, tutakuwa na ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na jimbo la Haryana.”

Kituo cha Uwekezaji Nchini kimeeleza kuwa huo ni mwanzo wa ushirikiano na jimbo la Haryna kutoka nchini India lakini pia kitaendelea kuvutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ili kukuza uchumi wa Mtanzania na taifa kwa ujumla.
Post a Comment

0 Comments