Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI RUVUMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaasa watanzania kutumia fursa ya mikutano ya kisiasa kufanya siasa za kistaarabu ili kuendeleza amani na utulivu uliopo nchini.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lilondo kilichopo halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wakati alipowasili kuanza ziara ya kikazi katika mkoa huo leo tarehe 20 Julai 2023.

Amesema si vema kutumia lugha zisizo na staha katika kufanya siasa kwani hupelekea uvunjifu wa hali ya amani na utulivu.

Makamu wa Rais amesema katika mwaka huu wa fedha serikali itajenga barabara ya Litukila - Songea kilometa 98 ili kukabiliana na changamoto za miundombinu mkoani humo.

Pia ameigiza wizara ya maji kupeleka shilingi milioni 150 katika Kijiji cha Lilondo zitakazowezesha usambazaji wa miundombinu ya maji ili kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.

Akiwa katika Kijiji cha Mlilayoyo kilichopo Namtumbo mkoani humo, Makamu wa Rais amekemea uingizwaji kwa wingi wa mifugo hususani ng’ombe hali inayochochea katika uharibifu wa mazingira.

Ameuagiza uongozi wa mkoa wa Ruvuma kufanya tathimini ya mifugo iliopo na uwezo wa mkoa huo katika kupokea ng’ombe hizo.

Makamu wa Rais amewataka wananchi wa mkoa huo kuwa makini wakati wa kuuza mazao hususani ya chakula ili kuhakikisha wanabaki na akiba ya kutosha.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

20 Julai 2023

Ruvuma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lilondo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wakati alipowasili mkoani humo kwaajili ya ziara ya kikazi. Tarehe 20 Julai 2023.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mlilayoyo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati alipowasili mkoani humo kwaajili ya ziara ya kikazi. Tarehe 20 Julai 2023.

Post a Comment

0 Comments