Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS AKIWA KATIKA HAFLA YA MAKABIDHIANO YA MADARASA BUHIGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanasimamia vema watoto wao kupata elimu kwa mustakbali wa Maisha yao na kuwa na uhakika wa wataalamu mbalimbali wa baadae kwa manufaa ya taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo leo 05 Julai 2023 wakati aliposhiriki hafla ya kukabidhi madarasa matatu, ofisi mbili na samani katika shule ya Muyama iliopo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, madarasa yaliokarabatiwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB).

Amesema serikali inaendelea na jitihada za kuboresha sekta ya elimu ikiwemo kuondoa ada kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, kuongeza madarasa na shule ili kuwa na mazingira rafiki ya upatikanaji wa elimu.

Pia Makamu wa Rais amewaagiza wananchi, walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Muyama kutunza vema majengo na samani katika shule hiyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu.

Amesema ukarabati wa majengo hayo unapaswa kwenda sambamba na utunzaji wa mazingira, ikiwa ni pamoja na usafi na upandaji miti ya aina mbalimbali kama vile ya matunda na kivuli.

Halikadhalika ametoa wito kwa Halmashauri ya Buhigwe kwa kushirikiana na wadau wengine kufikiria kuanzisha mashindano ya kila mwaka ya usafi na uhifadhi wa mazingira katika Shule za Msingi na Sekondari.

Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa wadau mbalimbali hapa nchini kujitokeza kuunga mkono juhudi za maendeleo ya jamii inayowazunguka hususan maeneo ya vijijini ambako mahitaji ni makubwa.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameahidi kuanzisha tuzo maalum zitakazoenda sambamba na zawadi kwa wanaofanya vizuri katika shule hiyo ya Msingi Muyama ambayo alipata elimu ya msingi mwaka 1968-1970 ili kuongeza ushindani na ari kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Muyama mara baada ya hafla ya kupokea Madarasa, Samani mbalimbali na Ofisi za Walimu yaliokarabatiwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) katika Shule ya Msingi Muyama iliopo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Tarehe 05 Julai 2023. (Wengine katika picha ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa Kigoma Thobias Andengenye, Mkurugenzi wa TCB Sabasaba Moshingi na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Muyama Stella Shayo)





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia mara baada ya kupokea Madarasa, Samani mbalimbali na Ofisi za Walimu yaliokarabatiwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) katika Shule ya Msingi Muyama iliopo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Tarehe 05 Julai 2023.





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa darasani pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Madarasa, Samani mbalimbali na Ofisi za Walimu yaliokarabatiwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) katika Shule ya Msingi Muyama iliopo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Tarehe 05 Julai 2023.





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati alikiwasili katika Shule ya Msingi Muyama iliopo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma kushiriki hafla ya kupokea Madarasa, Samani mbalimbali na Ofisi za Walimu yaliokarabatiwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB). Tarehe 05 Julai 2023.

Post a Comment

0 Comments