Ticker

6/recent/ticker-posts

MBUNGE AWASHUKIA WAPOTOSHAJI BANDARI


MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amewaomba watanzania kutokubali kupotoshwa na mtu yoyote kuhusu uwekezaji unaotaka kufanyika baina ya serikali ya Tanzania nay a Dubai na kusisitiza kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni njema na kamwe hawezi kuuza nchi.

Mtaturu amesema hayo Julai 14,2023,katika viwanja vya shule ya sekondari Ikungi wakati akizindua Mashindano ya East Singida Inter School Sports 2023,ambayo inahusisha shule 19 za serikali na binafsi zilizopo katika jimbo hilo ambapo pia amegawa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Shilingi Milioni 16.6.

Amesema yeye amekuwa kwenye kamati ya miundombinu tangu alipoingia bungeni kamati ambayo inasimamia sekta ya uchukuzi na katika kipindi chote wameona changamoto zilizopo.

“Ndugu zangu niwaombe msipotoshwe na mtu yoyote,ukiona mtu anakwambia eti ooh Rais ameuza nchi muulize kwa Sh ngapi,maana kitu chochote kinachouzwa lazima kiwe na bei ya mauziano,na kwa kuwa kazi yao ni kupotosha utaona mtaagana pale mtakunywa maji na kila mtu ataenda kulala nyumbani kwake ,”amesema.

KWA NINI TURUHUSU UWEKEZAJI.

Mtaturu amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanafaidika na udhaifu wa bandari uliopo ili wao wachukue fedha wapige dili na wawanyonye watanzania.

“Leo tunaenda kumpata mtu atakayefunga mifumo yote itakayoangalia wapi wameingiza kontena ,la nani,kwa gharama kiasi gani ,awali tulikuwa tunakusanya ushuru wa forodha Sh Trilioni 7 kwa mwaka lakini baada ya uwekezaji huu tutaenda kukusanya Trilioni 26 kwa mwaka ,maana yake Trilioni 44 ya bajeti yetu tutaenda kuibeba wenyewe sawa na asilimia 62,

“Hii maana yake tukiongeza mapato yatokanayo na uboreshaji wa shughuli za bandari tutaachana na mikopo ya masharti magumu pia tozo mbalimbali zinazowaumiza wananchi,leo kuna baadhi ya watu wanaleta misaada wanatupangia tuunge mkono ushoga kwa sababu amekupa kitu ili ukubaliane na masharti yake,mama Samia amesema hapana lazima tuwekeze wenyewe tuweze kuleta maendeleo ya watanzania,”ameeleza

Mtaturu ametolea mfano uwekezaji huo kama nyumba ambapo mmiliki anaamua kupangisha baadhi ya vyumba au kuweka fremu ya maduka.

“Bandari ni kama nyumba umepangisha chumba kimoja ama viwili,mbele umefungua fremu ya maduka unaweka wapangaji ili upate kodi,hivyo bandari hii ni lango la uchumi lazima uweke mtu ambaye mwenye tija atakayewekeza nan chi ipate fedha,”ameongeza.

Ametolea mfano uwekezaji wa Kampuni ya TICTS walioongoza bandari hiyo kwa miaka 22 ,ambapo walikuwa wanatoa Sh Bilioni 300 kwa mwaka kwa gati namba 5 mpaka namba 11.

“Tulivyoenda pale tukamtathimini TICTS tukaona kweli huko nyuma tuliona hela nyingi lakini kwa sasa tumeona ni malipo kidogo, lakini pia kulikuwa na malalamiko makubwa ya wafanyabiashara kucheleweshewa kushusha mizigo yao,

“Leo hii pale Dar es salaam pamoja na uwekezaji mdogo uliowekwa meli inaweza kuchukua siku 5 mpaka siku 7 ndio iweze kushusha mzigo na kila siku inachajiwa dola 25,000 sawa na milioni 58 kwa siku moja huyu mfanyabiashara ukimlipisha yeye ataongeza bei ya bidhaa na hukuIikungi itakuwa kuwa juu maana yake serikali inachofanya sasa ni kupata mwekezaji mwenye uwezo atakayetuongezea tija atakayewafanya wafanyabiashara wengi waje washushe mizigo kwetu,”

Amesema hiyo itasaidia kuweza kupata ushuru utakaowezesha kujenga shule,barabara na taa za barabarani kama ambavyo zinawashwa kwenye Mji wetu wa Ikungi.

AWAOMBA WATANZANIA KUUNGA MKONO RAIS SAMIA.

“Nawaomba watanzania tuendelee kumuunga mkono Rais Samia,tumuombee maana kuongoza nchi sio jambo dogo,nchi hii ni kubwa ina watu zaidi ya Milioni 61,anawaongoza wananchi wenye mitazamo tofauti ,wengine wana akili timamu lakini wengine kwa makusudi tu wanataka kumkwamisha Rais wetu,niwaombe sanaa hata hili jambo la bandari mnalolisikia ni jambo la kawaida,limeshafanyika na serikali nyingine,”amesema

Post a Comment

0 Comments