Ticker

6/recent/ticker-posts

MILIONI 17 ZATUMIKA NUNUA VIFAA VYA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU KAGERA

Na Shemsa Mussa. Kagera

JUMLA ya Kiasi cha Shiling Milion 17. Zimetumika kuwanunulia vifaa mbalimbali vya shule Wanafunzi 50 wenye ulemavu kutoka Wilaya sita za Mkoa wa Kagera ikiwemo viti mwendo na baiskeli za magurudumu matatu.

Vifaa hivyo ambavyo ni viti mwendo na baiskeli za magurudumu matatu (5), jozi za viatu 38 na sale za shule 40 vimetolewa na shirika lisilo la kiserikali la TEKLA linalohudumia watu wenye ulemavu.

Akizungumza kwenye hafla ya ugawaji vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amewataka wazazi kuwapeleka shule watoto wao wenye ulemavu akidai kuwa kutowapeleka shule ni kuvunja sheria na kuwakosesha haki ya msingi ya kupata elimu

“Kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakikiuka sheria ya kuwapeleka watoto wao wenye ulemavu kuanza shule ya msingi, kwa mzazi yeyote ambaye atabainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria, Serikali yetu imeweka mipango mizuri kwa ajili ya watoto wetu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kutosha na choo kwa ajili ya watoto wetu wenye ulemavu,” amesema Sima

Mtendaji Mkuu wa shirika la TEKLA, Mugisha Kasaju amesema wanafunzi waliopokea msaada huo ni kutoka katika shule za msingi Mgeza viziwi, Mgeza Mseto, Tumaini, Rubale, Ryamaholo na Buzi.

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mgeza Viziwi, Benson Rwechungura amesema wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu wana mwamko mdogo wa kuwapeleka watoto shule jambo ambalo linasababisha watoto hao kukosa haki ya kupata elimu.

“Tunakumbana na changamoto ya wazazi kuwa na mwamko mdogo wa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu,

“Mfano watoto wanapofunga shule baadhi ya wazazi hawaji kwa wakati kuwatafuta watoto wao shule kuwapeleka nyumbani na wanapofungua shule baadhi ya wazazi wanachelewa kuwarudisha shule kwa madai kwamba wanaanza kuwahudumia vifaa vya shule wale watoto wao ambao si wenye ulemavu,” amesema

Moja ya mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu, Autropia Benedicto amesema mtoto wake Merry Daudi (11) yupo darasa la awali shule ya msingi Mgeza Mseto ambaye ana ulemavu wa miguu kushikana na mikono miwili kupinda.

Amesema alikuwa anabebwa kutoka bwenini kwenda darasani lakini msaada huo wa kiti mwendo utamsaidia kupunguza adha ya kubebwa kila wakati.







Post a Comment

0 Comments